Mbunge wa Muheza (CCM) Hamis Mwinjuma ama Mwana FA amepongeza nia ya serikali kuruhusu wadau mbalimbali kushiriki katika makusanyo ya mirabaha ya wasanii hata hivyo ameonya migogoro mipya ikiwa hakutakuwa na mikakati madhubuti katika utekelezaji wa kusudio hilo.
Mwinjuma alitoa angalizo hilo baada ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul kuliarifu Bunge kuwa Serikali inampango wa kuruhusu watu binafsi na Taasisi kuanza kukusanya mirabaha.
Gekul amesema tayari mapendekezo yameletwa Bungeni kupita mswaada wa Sheria ya fedha ya mwaka 2022/23 na inapendekeza COSOTA kubaki na jukumu la kusimamia hati miliki wakati jukumu la ukusanyaji mirabaha likiwa la taasisi au wadau binafsi Collective Management Organizations (CMOs) .
“Swala hili lina maslahi makubwa ya kiuchumi na kunaushahidi wa migongano kadhaa katika maeneo ambayo CMOs zimewahi kuruhusiwa, Je serikali inamkakati gani wa kuepusha migogoro kati ya CMOs,” alihoji Mwinjuma.
Gekul amekiri kuwa Sheria hii ilivyoanza kutekelezwa sehemu zingine iliibuka migogoro, hata hivyo amesisitiza kuwa serikali itakaa na wadau wote ili kuwezesha maelewano na kuepusha migogoro.