Serikali ya Uingereza na Shirika la Utangazaji nchini humo huenda wakaingia katika mzozo mkali mahakamani kuhusu habari ambayo BBC inataka kupeperusha ambayo inaripotiwa itamuweka hadharani jasusi wa serikali hiyo.
Telegraph imeripoti kuwa mpango huo ungefichua utambulisho wa mfanyakazi wa ujasusi anayefanya kazi nje ya nchi, na inaeleweka kuwa kesi hiyo ni nyeti sana.
Hakuna upande ambao umesema maudhui ya programu, lakini wote wamethibitisha kuwa serikali ilikuwa ikitafuta zuio mahakamani.
Katika taarifa, BBC ilisema: “Mwanasheria Mkuu ametaja kesi dhidi ya BBC kwa nia ya kupata amri ya kuzuia uchapishaji wa habari inayopendekezwa na shirika hilo.
“Hatuwezi kutoa maoni zaidi katika hatua hii, zaidi ya kuthibitisha kwamba hatutafuatilia hadithi yoyote isipokuwa ilionekana kuwa ni kwa manufaa ya umma kufanya hivyo na kulingana kikamilifu na viwango na maadili ya uhariri wa BBC.”
Katika taarifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imesema: “Mwanasheria Mkuu ametuma maombi dhidi ya BBC.
“Itakuwa haifai kutoa maoni zaidi wakati kesi zinaendelea.”
Telegraph iliripoti kuwa Mahakama Kuu huenda ikasikiliza shauri hilo Alhamisi.