Serikali imeagiza wananchi na wawekezaji wanaoendelea kujenga katika eneo linalozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara kuacha mara moja ili kuruhusu wanyama kuendelea kuishi katika ikolojia hiyo bila kubugudhiwa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alipofanya ziara ya kikazi katika eneo hilo lililopo kwenye Kijiji cha Migungani B, Wilayani Monduli.
“Naelekeza uzio wote uliojengwa kuzunguka hili ziwa uvunjwe na mwekezaji yeyote tutakayemsikia anajenga uzio tutamchukulia hatua za kisheria” Masanja amesisitiza.
Aidha , Masanja amesema kumekuwa na migogoro mingi kati ya wananchi na hifadhi baada ya kuvamia maeneo ya wanyama inayopelekea wananchi hao kuvamiwa na wanyama wakali kama tembo na kuwaasa wananchi kuchagua maeneo mazuri ya kuishi.
“Ifike mahali wananchi wahamie kwenye maeneo ambayo watakaa bila kubughudhiwa” Masanja amesema.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo Mhe. Masanja amesema Serikali ina mpango wa kufanya tathmini ya mapito yote ya wanyama na wananchi wawe tayari kuyaachia ili kukuza utalii nchini Tanzania.
“Nakuelekeza Mkurugenzi fanyeni tathmini katika mapito yote ya wanyama ili kujua majengo na mali zote zilizopo ili tuwahamishe wananchi kwa kuwapa fidia ili wanyama hawa waweze kupita” amesisitiza Masanja.
Pia ameelekeza Maafisa Uhifadhi kufanya operesheni ya kuwatoa wanyama walio kwenye vizuizi vya kuta pembezoni mwa ziwa Manyara.
“Naelekeza maeneo yote yenye hawa wanyama kuwepo na ulinzi na ninaelekeza kabla mwezi huu haujaisha watoeni hawa wanyama walio kwenye vizuizi ili wawe huru” Masanja amesema.
Masanja amewataka wakazi wa kijiji hicho kushirikiana na serikali katika utunzani na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe amesema katika kikao cha awali kati yake na wahifadhi wamekubaliana wawe na kikao kila baada ya miezi mitatu ili kupitia maeneo yenye vibali vya ujenzi ili kutathmini kama eneo hilo ni ushoroba au la.
Amemtaka Diwani wa Kata ya Migungani Joseph Pareso kuwa na taarifa sahihi za watu wanaochukua ardhi katika eneo lake ili kuepusha migogoro inayojitokeza.
“Mheshimiwa Diwani lazima ajue nani amechukua ardhi, kiasi gani, maeneo gani na kwa sababu zipi” Frank amesisitiza.