MTANZANIA
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari ya Matui iliyopo Wilayani Kiteto, Mkoani Manyara Emmanuel Mbigima mwenye miaka 15 amefariki dunia baada ya kuchapwa viboko 12 na walimu wake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Christopher Fulme alisema mwanafunzi huyo alifariki dunia baada ya kuchapwa viboko na walimu wake watatu kutokana na kufeli somo la Kiswahili.
Mauaji hayo yalitokea juzi saa 4 asubuhi shuleni hapo na mwili wake kwa sasa unaendelea na uchunguzi.
Msemaji wa familia Emmanuel Ngowi alisema familia inataka kuona haki inatendeka juu ya kifo chandugu yao.
“Kwa kifupi mtoto wetu alikuwa haumwi na hakuwahi kulazwa hospitalini,, tunaomba haki itendeke kwani tunaona kuna mazingira ya kutaka kulindana na huenda haki isitendeke” Ngowi.
Chama cha Walimu Kiteto kimelaani tukio hilo na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kujua ukweli kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo.
Hata hivyo baada ya taarifa hizo kuzagaa mitaani kundi la wananchi wenye hasira kali walivamia kituo cha Polisi kwa lengo la kulipiza kisasi kwa kutaka kuwaua walimu hao.
NIPASHE
Madudu zaidi yameendelea kuibuka katika sakata la mabehewa feki 274 yaliyonunuliwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), na sasa imebainika kuwa kampuni iliyopewa zabuni ya kuleta mabehewa hayo ndiyo iliyokuwa ya bei ya juu zaidi kuliko kampuni 10 zilizokuwa zimeomba na haikuweka dhamana yoyote kama sheria ya manunuzi inavyotaka.
Imebainika pia kampuni ya Hindustan Engineering Ltd ya India, ambayo ilishinda zabuni hiyo, ilibadilishiwa vigezo, vya aina ya mabehewa kinyemela baada ya zabuni kutangazwa na wazabuni kuwasilisha maombi yao.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, kampuni hiyo iliomba kuiuzia TRL mabehewa 174 yenye ‘rubber’ badala ya ‘spring’Sh. bilioni 32.8 wakati kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd ya China ilikuwa tayari kuleta idadi hiyo ya mabehewa yenye viwango vinavyokubalika kwa Sh. bilioni 25.
Kampuni hiyo pia ilishinda zabuni hiyo ambayo ilihusisha kuleta mabehewa mengine 100 ya mizigo ambayo ni ya muundo wa matangi na yasiyofunikwa Sh. bilioni 18.5 wakati kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd ya China iliyokuwa ndiyo yenye bei ndogo ilikuwa tayari kuleta idadi hiyo ya mabehewa kwa Sh. bilioni 13.09.
Kampuni hiyo pia ilishinda zabuni ya kuiuzia TRL vipuri kwa thamani ya Sh. bilioni 4.4 baada ya kuirekebisha na taarifa ya zabuni inaonyesha kuwa iliwasilisha zabuni iliyorekebishwa na ilikubaliwa.’
Kampuni ya Baotou Beifang Chuangye Co. Ltd iliomba kuleta vipuri hivyo kwa Sh. bilioni 4.46 wakati kampuni nyingine kama Transnet iliomba kwa Sh. bilioni 5.6 wakati Modern Industries iliyoshindwa kwa kutowasilisha dhamana iliomba kwa Sh. bilioni 6.02.
Kwa ujumla taarifa zinaonyesha kuwa kampuni ya Hindustan Engineering ililipwa Sh. bilioni 55.9 wakati kampuni iliyokuwa ya bei ndogo kuliko zote ingeweza kufanyakazi hiyo kwa Sh. bilioni 43.86 hatua ambayo ingeokoa Sh. bilioni 12.02 na kutoitumbukiza nchi kwenye hasara hiyo ya mabehewa feki.
“Mabehewa nyenye rubber hayawezi kabisa kwa namna yoyote ile kupita kwenye reli yetu. Kilichotokea ni kwamba zabuni iliyotangazwa ilitaka wazabuni walete mabehewa yenye spring ambayo ndiyo sahihi, lakini baadaye inaonekana walibadilisha vigezo na kuielekeza kampuni waliyoipa zabuni vigezo vipya ndiyo maana unaona mabehewa yaliyokuja hayafai,” alisema mmoja wa wataalam wa reli ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kampuni ya Hindustan Engineering Ltd haikuweka dhamana yoyote jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma na ilitaka ilipwe fedha yote kabla ya kuingiza mabehewa nchini jambo ambalo TRL ilitekeleza.
Wakati mzabuni huyo akiweka masharti hayo, kampuni nyingine zilizoomba ikiwamo iliyokuwa ya bei ndogo zaidi, iliweka dhamana na ilitaka ilipwe kwa awamu hadi itakapokamilisha kazi husika.
NIPASHE
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma kujibu shtaka la kutumia lugha ya matusi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Hadija Nyembo.
Kafulila alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:00 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, David Ngunyale, Wakili wa Serikali, Maryasinta Lazaro, alidai kuwa Mbunge huyo alitenda kosa hilo Agosti Mosi, mwaka 2013, katika Kata ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Wakili huyo alidai kuwa Mbunge huyo alimtolea maneno ya matusi Nyembo kuwa hana maadili, ana akili finyu na ni kiumbe dhaifu, kitendo ambacho kingesababisha uvunjifu wa amani.
Wakili Lazaro, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba kupangwa tarehe nyingine ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Ngunyale alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 19, mwaka huu.
Wakili wa Mbunge huyo, Danieli Rumenyela, aliomba Mahakama hiyo kumpunguzia mteja wake masharti ya dhamana ili kumalizia vikao vya Bunge ambavyo vinatarajia kuanza mwezi ujao.
Hata hivyo, Kafulila alikana shtaka hilo na kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kata na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni mbili kisha kuachiwa.
Kafulila alidhaminiwa na Diwani wa Kata ya Katubuka (Chadema), Moses Bilantanye.
Kabla ya kufikishwa mahakamani jana, Mbunge huyo alikuwa nje kwa dhamana ambayo alipewa na askari wa kituo cha Polisi Kati baada ya kudaiwa kumtukana Mkuu huyo wa wilaya.
MWANANCHI
Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM na kwamba ile yenye upinzani itaandikishwa kwa kulipua ili watu wengi wenye sifa ya kupiga kura wasiandikishwe.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva amesema hilo ni jambo jipya kwake kwa kuwa hawakuangalia suala hilo wakati wa kupanga mikoa hiyo.
Akizungumza jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili nchini akitokea Marekani, Dk Slaa alisema wamegundua kwamba mwishoni mwa kazi ya uandikishaji kwenye mikoa ambayo ni ngome ya vyama vya upinzani, watu wengi hawataandikishwa.
“Tumegundua hujuma zao, NEC wameanza kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM. Huko wanajitahidi kuandikisha wapigakura wote na wanachukua muda mrefu,” Dk Slaa
“Mikoa yenye ngome ya Chadema na vyama vingine vya upinzani itakuwa ya mwisho kuandikisha wapigakura na uandikishaji huo utakuwa wa harakaharaka ambao utawaacha mamia ya watu bila kuandikishwa kwa sababu muda utakuwa hautoshi,” Dk Slaa.
Alisema suala hilo linaweza kuvuruga uchaguzi, hasa ikizingatiwa kwamba mchakato wa uandikishaji umekuwa na sintofahamu nyingi.
MWANANCHI
Mlinzi wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alijisalimisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili ya kukutwa na bastola aina ya Berretta pamoja na risasi 20 kinyume na sheria.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobera kuwa baada ya kuomba mahakamani hapo hati ya wito ya kumuita mshtakiwa George Mzava , jana alijisalimisha akiambatana na Wakili Peter Kibatala.
Akimsomea hati ya mashtaka, Kweka alidai kuwa Machi 29 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, akiwa na wenzake Bihagaze na Milulu walikutwa na bastola aina ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali cha mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.
Alidai kuwa washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume cha Sheria ya Silaha.
Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio, Mzava akiwa na wenzake hao walikutwa wakimiliki isivyo halali, risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya shotgun.
Mshtakiwa huyo baada ya kusomewa mashtaka hayo aliyakana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika.
MWANANCHI
Raia 12 wa Iran na Pakistan wanaokabiliwa na shtaka la kuingiza nchini shehena ya mihadarati yenye thamani ya bilioni 9 wamesema kuwa kama upepelzi wa kesi zao haujakamilikni bora wapigwe risasi wafe kuliko kukaa mahabusu kwa muda mrefu.
Walitoa malalamiko yao jana mbele ya hakimu Janeth Kaluyenda baada ya wakili wa Serikali Janeth Kitali kudai kuwa upelelezi wao haujakamilika na kesi imeahirishwa mpaka Mei 4.
Raia hao walikamatwa katika bahari ya Hindi upande wa Tanzania wakiingiza shehena ya kilo 200.5 za dawa za kulevya aina ya Heroin.
Kesi hiyo ipo mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa na upepezi ukikamilika itahamishiwa mahakama kuu Tanzania kanda ya Dar es salaam.
MWANANCHI
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amebainisha sababu nne zinazowafanya wananchi wampendekeze kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Nchemba aliyasema hayo jana kwenye mahojiano wakati wa kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na ITV kuhusu tafiti zinazofanywa juu ya kukubalika kwa baadhi ya watia nia ya urais miongoni mwa wananchi wanaomtaja.
“Nisingependa kuwa refarii na mchezaji kwa wakati mmoja katika hili. Kuna ripoti iliwahi kuonyesha kuwa ninaongoza katika mbio hizo kwa kupata asilimia 37 na nyingine ikasema nimeshika nafasi ya pili. Ninawashukuru wananchi wanaoona kuwa nafaa katika nafasi hiyo.”
Aliongeza: “Wanaonipigia kura wanaona nidhamu katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, matumizi. Pia mabadiliko ya kukomesha ufanyaji kazi wa mazoea.”
Tangu ateuliwe kushika wadhifa wa Unaibu Waziri, Nchemba alisema amefanya mabadiliko kadhaa ambayo yamesaidia kudhibiti matumizi ya Serikali, ikiwamo kupitisha malipo ya wafanyakazi wote wa serikali katika akaunti zao za benki.
Sambamba na hilo aliagiza wakuu wa idara wote kuhakiki taarifa za watumishi walionao katika ofisi zao jambo lililochangia kuokoa zaidi ya Sh400 milioni zilizokuwa zinalipwa kwa waajiriwa hewa.
Pamoja na hayo alisema kuwa, kwa sasa amejikita zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya unaibu waziri.
Alipoulizwa anachukuliaje kufananishwa na aliyewahi kuwa waziri mkuu katika utawala wa awamu ya kwanza, Edward Sokoine, alijibu kuwa hiyo ni ishara nzuri kwani kiongozi huyo alitukuka katika utumishi wa umma.
“Hilo linanifanya nitende kulingana na mahitaji ya wananchi. Uongozi wa Sokoine ulipendwa na wengi na kufananishwa na kiongozi aliyetukuka kama yeye ni sifa nzuri inayoniongezea ari,” alisema.
Akizungumzia mtindo wake wa kuvaa skafu ya bendera ya Taifa alisema, anatazamia kuwa baada ya muda mfupi itakuwa ni utambulisho wa taifa kwa kila Mtanzania atakayeenda nje ya nchi.
“Nilianza kuvaa skafu tangu nikiwa sekondari…wakati huo zenye rangi za bendera ya taifa hazikuwa nyingi lakini kadri siku zinavyosogea zinaongezeka.
HABARILEO
Serikali imefanikisha kurejea nchini kwa kundi la pili la Watanzania 14 wanaoishi Yemen, ambako kuna machafuko ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Watu hao wameelezea jinsi walivyoteseka na kuathirika kisaikolojia, huku wakiwataka Watanzania waliopo nchini, kutojaribu kuichezea amani iliyopo.
Katika kuyanusuru maisha yao, Watanzania hao waliogharamia chakula, malazi na usafiri wa kurejea nchini, wamesema walilazimika kutangatanga kwa zaidi ya wiki mbili na hatimaye kufanikiwa kurejea salama nchini.
Kurejea kwao jana, kumefanya watanzania waliorejea nchini hadi sasa kutoka Yemen kufikia 39, kati ya 64 waliopo nchini humo.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam baada ya kurejea na ndege ya Shirika la Ndege ya Emirates, watanzania hao walisema kama sio juhudi za serikali ya Tanzania, wana uhakika kwa sasa wangekuwa wafu.
“Sina cha kusema, kwa kweli naishukuru serikali yangu na Balozi wangu kule Muscat, Oman alitusaidia sana, nilikuwa naishi Yemen mimi na familia yangu ya watu 10, na hali ilipozidi kuwa mbaya niliomba msaada ubalozini na walitusaidia na tumerejea nyumbani na familia yangu kwa gharama za serikali, hili sio jambo dogo,” Sabri Abeid Almaghi.
Akisimulia hali halisi nchini Yemen, Almaghi alisema tangu mwaka 2011 amekuwa akiishi nchini humo yeye na mkewe na familia yake ya watu 10, akifanya biashara ya maduka ya kuuza vipuri vya pikipiki na kwamba hali ya siasa ikachafuka na mapigano yakaanza.
Alisema baada ya machafuko kutokea, ilimbidi afunge maduka yake na kuhamishia vipuri vyote kwenye stoo moja na kisha kurudisha maduka ya watu aliyokuwa amepanga na kuanza kutafuta msaada ubalozini wa kurejea nyumbani.
“Kwa kweli kule hivi sasa ni taabu tupu, hali sio nzuri kwanza uwanja wa ndege ulifungwa, tukaambiwa muda unavyokwenda barabara nazo zitafungwa, nilikuwa ninaishi mji uitwao Mukalla, baada ya kuona hali mbaya nilipiga simu ubalozini, kuomba msaada na ndipo tukaanza safari ya kuondoka Yemen kwa basi kwenda Muscat, tumechukua zaidi ya siku tano kusafiri,”Almaghi.
Aliongeza kuwa, kwa ujumla tangu walipoanza safari ya kuondoka Yemen hadi kufika Tanzania wakiwa salama jana, wametumia zaidi ya siku 15, jambo ambalo aliloelezea kuwa limempa uchovu mkubwa hasa kwa kuwa alikuwa na watoto na watu wengine wa familia yake.
HABARILEO
Kumeibuka vikundi vya watu jijini Dar es Salaam vikidaiwa kujichukulia madaraka ya kukusanya ushuru katika vituo vya daladala na kwa wafanyabiashara kwenye maeneo yasiyoruhusiwa hali ambayo mamlaka zinazohusika na usimamizi zimeshauriwa kuingilia kati kukomesha vitendo hivyo.
Kuhusu vituo vya daladala, lipo wimbi la wapigadebe ambao wanadaiwa kuhodhi vituo hivyo kwa kulipisha ushuru daladala, bajaj, pikipiki na hata magari ya watu binafsi yanayoamua kupakia abiria vituoni.
Kwa upande wa wamachinga, suala hilo linadaiwa kujitokeza zaidi katika eneo la Ubungo ambako liko kundi linalojiita ‘Matembo’ linalodaiwa kulipisha ushuru wa Sh 500 kwa kila mfanyabiashara ndogo aliye katika eneo hilo.
Vikundi vyote hivyo vilivyoamua kujichukulia mamlaka ya kutoza ushuru, vinashutumiwa kutumia nguvu na vitisho kujipatia fedha kutoka kwa wahusika. “Usipolipa shilingi mia tano, wanakufanyia fujo.
Wanakuvunjia meza. Ni wababe lakini hatuna jinsi ya kufanya. Tunawapa tu,” alisema mmoja wa wafanyabiashara katika eneo la Ubungo karibu na kituo cha zamani cha daladala aliyekutwa na mwandishi akizozana na wakusanya ushuru hao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo hilo la Ubungo, wapo wafanyabiashara wapatao 200, hali ambayo inakadiriwa kwamba, kikundi hicho hukusanya zaidi ya Sh milioni moja kwa siku kwa kisingizio cha kufanya usafi.
Mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema, kikundi hicho kinaundwa na watu wapatao saba ambao wamekuwa kero kubwa kwao.
“Hakuna usafi wanaofanya,Hawa ni wezi tu, wameamua kujitengenezea njia ya kuchukua fedha zetu, wao wamekaa tu wanasubiri kutulazimisha kuwapa hela,” alisema.
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mholela alipoulizwa iwapo wafanyabiashara katika eneo sanjari na watu wanaotumia mwanya huo kujikusanyia fedha kwa kutoza ushuru, alisema hawezi kukiri uwepo wa kikundi hicho.
Alisema anachofahamu ni kwamba, uwepo wa wafanyabiashara hao ni kinyume cha sheria kwa sababu tayari walishawaondoa na sasa wamerudi kinyemela.
millardayo.com ni sehemu yako utakapozipata zote unazozitaka, vichekesho, stori za siasa, muziki, michezo, movies, magazeti, video mpya na nyingine kubwa…. unaweza kujiunga na mimi Facebook, Twitter na Instagram pia zitakufikia zote mtu wangu, jiunge hapa >>>twitter Insta Facebook