Siku 17 baada ya madereva wa mabasi mchini kugoma na kutikisa nchi, Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (TABOA) kimetangaza mgomo mwingine nchi nzima.
Mgomo wa Aprili 9, mwaka huu uliodumu kuanzia alfajiri hadi saa 7:00 mchana ulitikisa nchi na kuwaathiri abiria wengi waliokuwa wanasafiri kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.
Jana Taboa walitangaza kusitisha utoaji huduma kuanzia kesho ikiwa ni hatua ya kupinga nauli mpya za mabasi zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
Kufuatia hali hiyo, Taboa kimewataka mawakala kutokatisha tiketi kuanzia leo kwa abiria hadi hapo Sumatra itakapotoa taarifa za kuruhusu nauli ya zamani ziendelee kutumika.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alitoa taarifa hiyo jana wakati akitoa majumuisho ya mkutano mkuu wa dharura uliojumuisha wadau wa usafirishaji.
Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu tatu ambazo ni ajali za barabarani, nauli mpya zilizotangazwa na Sumatra, madaraja ya mabasi, mgomo wa madereva na vituo vya kubadilishia madereva wanaokwenda umbali mrefu.
“Kesho hakuna gari ambalo litatoka kituo cha mabasi Ubungo kwenda mkoani na kama tutapigwa mabomu tupigwe, ila msimamo wetu uko pale pale wa kutotoa magari hadi Sumatra watakapotoa tamko la kutaka nauli za awali ziendelee kutumika,” alisema.
Kuhusu ajali, alisema kutokana na kukithiri kwa ajali za mabasi, wanakubaliana na utaratibu uliowekwa na serikali wa madereva kubadilishana wanaokwenda masafa marefu katika vituo ambavyo vitatengwa ili kupunguza ajali hizo.
MWANANCHI
Kiganja cha mtoto Baraka Cosmas mwenye ulemavu wa ngozi kilichokatwa Machi 8 kwenye kijiji cha Kipeta Sumbawanga kimepatikana mwishoni mwa wiki Wilayani Mbozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi alisema kiganja hicho kilipatikana kutoka kwa mkazi wa kijiji cha Malonje Sajenti Kalinga ambaye anafanya kazi ya Useremala.
Alisema awali walimkamata mganga mganga wa kupiga ramli ambaye ndiye aliyehusika kukata kiganja hicho na baada ya kumbana Mganga huyo alimtaja Kalinga ndiye aliyemtuma kuleta kiganja hicho cha albino.
“Tulimbana mtuhumiwa akatuambia aliyemtuma ni Kalinga kwa dau la milioni 100” Msangi.
“Polisi walifika kwa mtuhumiwa Kalinga na walipomuhoji kwa kina alikitoa kiganja hicho na kuwakabidhi”
Hadi juzi watu sita walishikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo wakiwemo waliokamatwa mwaka jana na wengine mwaka huu.
MWANANCHI
Helkopta ya Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, imeleta kizaazaa, baada ya Kada wa CCM, Buni Ramolle ambaye aliikodi kwa ajili ya mikutano yake ya kutangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo, kudai kuwa ni mbovu na ilitaka kumuua.
Kada huyo akaenda mbali na kueleza kuwa kutokana na hitilafu hiyo, ameitaka kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd, iliyomkodishia helkopta hiyo, kumrejeshea fedha zake zote alizoilipa kwa ajili ya kuitumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, Ndesamburo ambaye ni mmiliki wa helkopta hiyo kupitia kampuni yake ya Keys Aviation, alikanusha madai hayo akisema kuwa hayana msingi.
“Anasema helikopta ni mbovu wakati ilimpeleka na kumrudisha? Alihoji Ndesamburo na kusisitiza kuwa “tutawaomba wakaguzi wa ndege waifanyie ukaguzi na ripoti hiyo ndio tutaitumia kumshitaki nayo.”
Kuhusu madai ya Ramolle kuwa amerejeshewa fedha zake alizolipa, Ndesamburo alihoji “Tunamrudishia fedha gani wakati hakulipa? Kuwa na Proforma Invoice ndio kulipia?”
Awali taarifa zilieleza kuwa Ramolle alitoa tuhuma hizo, baada ya viongozi wa CCM, kumbana wakimtaka aeleze kwa nini ameamua kutumia helkopta ya Ndesamburo ambaye ni mpinzani wake kisiasa.
Lakini tayari Ndesamburo mwenyewe ameshajitokeza hadharani na kudai kuwa helkopta hiyo ni mali yake na kwamba ameingia mkataba wa kuikodisha kwa kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd.
Kwa mujibu wa Ramolle, kinachofanyika sasa ni mbinu za kumchafua ndani ya chama ili asiaminike na aenguliwe kama alivyoenguliwa mwaka 2010.
Ramolle alisema kutokana na Ndesamburo kudai helkopta hiyo ni yake, tayari kampuni ya General Aviation Services wamemrudishia fedha zake alizokuwa amekodishia na ameishtaki kampuni hiyo kwa Meneja wa TRA mkoa wa Kilimanjaro kutokana na kutompa risiti ya malipo aliyoyafanya.
MWANANCHI
Mwanasiasa na mkongwe aliyewahi kuwa waziri katika Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, Njelu Kasaka amekishauri chama chake cha CCM kuwaruhusu wanachama wanaotaka kuwania urais kujitangaza ili kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kuwachambua na hatimaye kumpata kiongozi bora mwenye uwezo wa kuongoza nchi.
Chama hicho tawala, kimewapiga ‘kufuli’ makada wake sita, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kwa madai ya kufanya kampeni mapema.
Lakini ushauri huo wa Kasaka, aliyewahi pia kuwa mkuu wa mkoa, umetulipiwa mbali na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye ambaye amesisitiza kwamba hawawezi kufuata maoni hayo, bali wataendelea na utaratibu wa vikao katika kumpata mgombea wake.
Nape alisema: ‘‘Chama kina utaratibu wa vikao na ndiyo utakaofuatwa. Maoni ya Njelu Kasaka ni haki yake.” Alipoulizwa ni lini vikao vya uteuzi vitaanza, alijibu kwa mkato “bado.”
Akizungumza kwa simu jana, Kasaka alisema hivi sasa hatua ya kujitangaza imecheleweshwa na kwamba kinachotakiwa ni ifikapo Julai mwaka huu, mgombea urais awe ameshapatikana baada ya wananchi kumpima uwezo wake.
“Hatuwezi kuambiwa na mtu mwingine uwezo wa mgombea urais, bali tunataka kusikia kutoka kwake kwani atatakiwa kututhibitishia yeye mwenyewe na wananchi wakamsikiliza na kumpima kuona kama anakidhi kuendesha nchi na kukabiliana na matatizo tuliyonayo,” alisema.
Kasaka alisema hatua ya wagombea kuchelewa kujitangaza italeta athari itakayokigharimu chama chake na nchi kwa ujumla huku akisema ni vigumu kumpata kiongozi bora atakayekuwa ameteuliwa na viongozi pekee.
Alisema kuwa CCM itamtoa mgombea anayekubalika, aliyefuata maadili, taratibu na kanuni za chama katika utekelezaji wa majukumu yake.
MWANANCHI
Koplo Laura Mushi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ni miongoni mwa Watanzania 42 waliotunukiwa nishani na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu juzi Dar es Salaam.
Laura alitunukiwa Nishani ya Ushupavu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika hafla hiyo Rais Kikwete alitunuku Nishani ya Kumbukumbu ya miaka 50 ya Muungano Daraja la Pili, la Tatu na la Nne, Nishani ya Muungano Daraja la Pili na Nishani ya Ushupavu.
Kabla ya kupokea nishani hiyo, ilielezwa kwamba usiku wa Machi 14 mwaka huu, Koplo Laura , akiwa kwenye kituo chake cha ulinzi, alivamiwa na kundi la majambazi waliomkaba kwa kamba na kumburuza kwa lengo la kutaka kumuua na kupora bunduki aliyokuwa nayo ikiwa na risasi 30.
Ilielezwa kwamba wakati majambazi hao wakimburuza kutoka katika lindo lake, Koplo Laura alijitahidi na kufanikiwa kudhibiti kamba hiyo isimnyime pumzi kwa kuwa walikwisha mfunga shingoni, huku akipambana kuzuia asinyang’anywe bunduki aliyokuwa nayo na kufanikiwa.
Alifanikiwa kuidhibiti kamba hiyo na kisha kuifikia chemba ya risasi ya bunduki na kuweza kufyatua risasi nne huku akiburuzwa.
Hali hiyo iliwafanya majambazi hao kumwachia na kukimbia, hivyo kuokoa maisha yake na silaha aliyokuwa nayo.
“Kitendo hicho kimeonyesha ushupavu, uzalendo na heshima ya hali ya juu kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wanawake wote nchini,” alisema mshereheshaji wa shughuli hiyo.
Akizungumza baada kupokea tuzo hiyo, Koplo Laura alisema: “Sikutarajia kupata nishani hii, imenitia moyo, nguvu na morali zaidi wa kufanya kazi kuilinda nchi yangu, pia kuonyesha kwamba inawezekana kila palipo na juhudi. Ninamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kutambua mchango wangu.”
Katika hafla hiyo, watu wengine wa kada mbalimbali wakiwamo wanasiasa, watumishi wa umma pia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wastaafu na majaji wastaafu walitunukiwa nishani.
Kupitia nishani hizo, Rais Kikwete pia amemkumbuka marehemu Brigedia Jenerali Moses Nnauye aliyekuwa Katibu wa Oganaizesheni wa CCM na mwasisi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliyetunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Tatu.
HABARILEO
Serikali imetenga Sh bilioni tisa kwa ajili ya posho ya kujikimu na nauli kwa ajili ya walimu 31,056 na mafundi sanifu maabara 10,625, ambao ajira zao zimetangazwa jana huku wakitakiwa kuanza kazi Mei Mosi mwaka huu.
Aidha, watumishi hao wapya, wamehadharishwa juu ya ucheleweshaji, wakiambiwa kwamba, atakayeripoti mwisho wa mwezi wa Mei, hatapokewa isipokuwa, kama ana matatizo yanayotambulika.
Wakati kawaida walimu wapya hupangiwa halmashauri ambazo ndizo zenye jukumu la kuwapangia vituo vya kazi, kwa upande wa walimu wa sekondari wa masomo ya Sayansi na Hisabati ambao idadi yao ni 2,700, wamepangwa moja kwa moja kwenye shule ambazo hazina walimu.
Hayo yalibainishwa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini alipokuwa akielezea kile alichosema ni sababu za kiufundi za kushindwa kutangaza majina ya ajira mpya za walimu Aprili 24, mwaka huu kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
Katika kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa wa walimu na wanafunzi, halmashauri zilizojitosheleza au zenye idadi ya kuridhisha ya watumishi hao, hususani za mjini, hazikupangiwa kabisa walimu.
Posho Alisema fedha hizo ambazo ni posho ya kujikimu kwa siku saba na fedha za nauli zinatakiwa kulipwa na halmashauri ambao ni mwajiri. Zinatakiwa kulipwa ndani ya siku saba bila kuzidi siku 14 tangu kuripoti kwa mtumishi katika kituo cha kazi.
“Mwenye jukumu la kutuma fedha kwenye halmashauri ni Wizara ya Fedha. Lakini tumeziambia halmashauri zihakikishe zinalipa walimu ndani ya siku 14 tangu kuripoti na tuna uhakika kwamba halmashauri zina fedha,” alisema.
Alisema upo mfumo katika Tamisemi, ambao unaangalia fedha zilizoko katika halmashauri jambo alilosisitiza kwamba wanao uhakika kwamba zipo kuwezesha malipo hayo.
HABARILEO
Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kwa kuwa umepitia taratibu zote. Pia, Ikulu imesisitiza kuwa sheria hiyo ni nzuri na itadhibiti matumizi mabaya ya mtandao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alitoa taarifa hiyo jana, alipozungumza na waandishi wa habari, Ikulu jijini Dar es Salaam. Rweyemamu alisema sheria ya Makosa ya Mtandao itasainiwa na rais muda wowote.
“Hii ni sheria nzuri, kwanza inadhibiti matumizi mabaya ya mitandao, wote watakaohusishwa ama kutuma au kutumiwa vitu au picha mbaya sheria itawabana wote, na kama umetumiwa bila idhini yako, toa taarifa polisi, ili uwe kwenye upande salama,” Rweyemamu.
Alisema madai ya wadau kwamba inanyima uhuru wa kupata taarifa, hayako sahihi kwa kuwa hiyo si sheria ya habari.
Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ulipitishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge, uliofanyika Dodoma hivi karibuni. Katika mjadala, wabunge wengi walikemea vitendo vilivyokithiri vya uhalifu wa mtandao nchini, na kutaka sheria hiyo itakaposainiwa, itumike ipasavyo kudhibiti.
Wabunge wengi walisema viongozi, watu maarufu na jamii kwa ujumla, wamekuwa waathirika wakubwa wa matumizi hayo mabaya ya mtandao, kutokana na kutukanwa, kutishiwa kuuawa, kuzushiwa uongo na hata wakati mwingine kutapeliwa.
Hata hivyo, baada ya kupitishwa muswada huo, kumekuwapo na kauli za ukosoaji kutoka kwa watu binafsi na makundi mbalimbali, wakitaka rais asisaini hadi baadhi ya vifungu virekebishwe.
Miongoni mwa mambo yaliyokosolewa ni pamoja na sheria kubana pia mtu anayetumiwa vitu au picha mbaya . Wakati huo huo, Rweyemamu akizungumzia Muswada wa Sheria ya Takwimu kuhusu maombi ya wadau ya kutaka ziangaliwe pande zote mbili wakati wa kutiwa hatiani, kutokana na kutoa au kuandika takwimu zisizo sahihi. Alisema maombi hayo yatazingatiwa.
MTANZANIA
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, amekana kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.
Amedai kwamba alichozungumza kiliungwa mkono na viongozi wa juu wa chama hicho akiwamo John Malecela na Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya.
“Si kweli kwamba maneno niliyotoa yalikuwa yanawakashifu walalamikaji na kuwaathiri hadi kuwasababishia madhara,” alidai.
Makonda anadai kwamba walalamikaji walitakiwa kufuata katiba, kanuni na taratibu zilizowekwa ndani ya chama kwa kuwasilisha malalamiko hayo ndani ya chama badala ya kukimbilia mahakamani.
Mdaiwa huyo mwishoni aliiomba mahakama kuyatupa madai yaliyopo dhidi yake kwa gharama.
Mahakama iliwapa nafasi walalamikaji kuwasilisha hoja za nyongeza kama zipo Mei 5, mwaka huu na kesi hiyo itatajwa Mei 11, mwaka huu.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Msindai na Guninita wanaiomba mahakama hiyo imwamuru Makonda awaombe msamaha na kuwalipa kila mmoja Sh milioni 100.
Msindai na Guninita wanaotetewa na Wakili Benjamini Mwakagamba, wanaiomba mahakama pamoja na mambo mengine itoe zuio la kudumu kwa Makonda asizungumze tena maneno ya kashfa wala kuyasambaza kama alivyofanya awali.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza>>> twitter Insta Facebook