Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeshindwa kumhoji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, kutokana na mwenendo wa afya yake.
Jana Mwanasheria wa askofu huyo Paul Mallya akiambatana na Askofu Gwajima akiwa kwenye baiskeli ya magurudumu mawili ya kubeba wagonjwa, walifika katika Kituo Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam saa 2.00 asubuhi kwa ajili ya kuitikia wito wa polisi uliotaka Askofu huyo akahojiwe.
Hata hivyo, kabla hajamaliza kupandishwa ngazi ya pili kuingia kwenye jengo la ofisi za kituo hicho, polisi walisema hawawezi kumhoji mpaka afya yake itakapoimarika.
“Tulifika kituo kikuu cha polisi saa 2.00 asubuhi tukiwa tayari kwa mahojiano. Askofu alipoanza kupandishwa ngazi akiwa katika baiskeli ya magurudumu mawili ya kubeba wagonjwa, polisi walipomuona, kabla hajamaliza kupanda, walitwambia ni vyema akarudi nyumbani mpaka Aprili 9, mwaka huu ndipo wamhoji,” alisema Mallya.
Alisema kuna mtu aliyetambulika kwa jina la Abubakar Yusufu, mkazi wa Kiluvya, wilaya ya Kisarawe, mkoa wa Pwani, ndiye amefungua kesi ya jinai polisi akilalamika kukwazwa na lugha iliyotumiwa na Askofu Gwajima dhidi ya Askofu Mkuu Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.
Askofu Gwajima alifika katika kituo hicho akisindikizwa na msafara wa magari matatu.
Gari la kwanza lilimbeba Mchungaji Baraka; la pili, aina ya Land Cruiser alikuwamo Askofu Gwajima na la tatu lilikuwa lake (Mallya).
Tofauti na ilivyokuwa Jumanne kwa wafuasi wengi wa Askofu Gwajima kufurika katika kituo hicho na kulilazimisha Jeshi la Polisi liimarishe ulinzi kwa ajili ya kuwadhibiti, jana hawakuwapo.
Jana Askofu huyo hakuzungumza chochote badala yake Mallya ndiye aliyezungumza kwa kifupi na waandishi.
Mallya alisema Askofu Gwajima amefunguliwa mashtaka ya jinai yanayohusisha kutumia lugha kumkashifu Kardinali Pengo.
Alisema Yusufu alifungua mashtaka hayo kutokana na picha ya video aliyoiona kwenye mitandao ya kijamii inayomuonyesha Askofu Gwajima akitumia lugha ya matusi kumkashifu Askofu Pengo ambayo kisheria ni kosa.
Machi 26, mwaka huu, Jeshi la Polisi Kanda hiyo lilimwamuru Askofu Gwajima kujisalimilisha polisi kwa tuhuma za kumkashifu Kardinali Pengo.
Baadaye, Machi 27, Askofu Gwajima alijisalimisha kituo hicho lakini wakati akihojiwa alizimia akiwa chumba cha mahojiano kisha kukimbizwa katika Hospitali ya TMJ kwa matibabu.
NIPASHE
Shinikizo la kumshawishi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuchukua fomu ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu, limeendelea na safari hii wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya jijini Mwanza, wakitoa tamko la kumtaka kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, viongozi wa vyuo vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo Kikuu Katoliki cha Sayansi na Tiba za Afya (CUHAS), walimtaka Lowassa kuchukua fomu ya kuwania urais wakati ukifika.
Viongozi hao waliyazungumza hayo wakati wakikabidhi misaada mbalimbali kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Upendo Daima, jijini Mwanza.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa CUHAS, Godfrey Kisigo, alisema wameamua kumuunga mkono Lowassa kwa sababu anapendwa na kila Mtanzania.
Alisema wanamuomba muda ukifika awe mtu wa kwanza kujitokeza kuchukua fomu ili kugombea nafasi ya urais.
“Tamko hili ni la vyuo vikuu vyote vya Mwanza, sauti zetu ni za busara kwa sababu zinataka kuikomboa nchi yetu kwa miaka 10 ijayo, tunayo imani kubwa na Lowassa katika hatma ya nchi hususan elimu kwa watu wote,” alisema na kuongeza:
“Hatma ya nchi hii ipo mikononi mwako na sisi wanavyuo hatuwezi kusubiri kuona tunakosa kiongozi atakayelisaidia Taifa kwa kuzibwa midomo, tupo tayari kufa ili uwe rais uokoe watakaobaki na Tanzania.”
Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi SAUT, Christopher Mkodo, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisijaribu kukata jina la Lowassa kwani Tanzania bila kiongozi huyo Watanzania watakuwa wamenyimwa fursa ya kupata maendeleo ndani ya miaka 10.
Waliitaka CCM kusikiliza maoni ya wanachama wake vinginevyo chama kitaharibika.
Mwakilishi wa CBE, Paul Dotto, alisema Lowassa ni chaguo la wanafunzi wa vyuo vikuu na wana imani ataifikisha Tanzania katika uchumi wa kati kabla ya malengo yaliyowekwa na Serikali.
NiPASHE
Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwamba anawaburuza wabunge wa upinzani kwa sababu hawafuati utaratibu bungeni.
Makinda alisema hayo alipokuwa akiwajibu wabunge wa upinzani waliolalamika kuburuzwa baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuomba majibu kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu kura ya maoni.
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi a CUF Taifa, Abdul Kambaya, alisema kauli hiyo ya Makinda ni ya dharau, ambayo hazipaswi kutolewa, hasa na kiongozi wa wabunge.
“Spika Makinda anakuwa chanzo cha vurugu bungeni, hasa kwa kuwa mtetezi wa serikali bungeni, badala ya kuwa kiongozi wa Bunge asiyeegemea upande wowote,” Kambaya.
Alisema kitendo cha Spika Makinda kulazimisha kusomwa miswada miwili kuhusu habari na matumizi ya mitandao ya kijamii, hakikubaliki kwa Watanzania na kinadhihirisha kishachoka kuliongoza Bunge.
“CUF tunamuonya Spika Makinda aache ukada wa CCM na kuiegemea serikali wakati maslahi ya wananchi yanavunjwa na kukanyagwa,” Kambaya.
Alimtaka Spika Makinda kutambua kuwa iwapo ataendelea na utaratibu huo, atalivuruga Bunge na kutowesha amani.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekubali kuahirisha upigiaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kutokana na kutokamilika kwa uandikishaji wa Daftrai la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo mfululizo wa matamko na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa demokrasia kwamba zoezi hilo lisingewezekana kwa sasa hasa kutokana kusuasua kwa mwenendo wa BVR.
Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu Damian Lubuva aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuwa kazi ya uboreshaji daftari la wapiga kura ni ya msingi kabla ya taratibu zote za upigaji kura.
Jaji Lubuva aliyeonekana kuwa mpole zaidi, alisema kwa uzoefu walioupata Njombe, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura bado halijakamilika katika mkoa huo na mingine iliyosalia.
“Hivyo tume haitaweza kuendelea na zoezi la upigaji kura ya maoni na zoezi hilo lililotangazwa hapo awali kufanyika Aprili 30, 2015 limeahirishwa hadi tarehe itakapotangazwa na Nec baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,” Jaji Lubuva.
Kwa nyakati tofauti, vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wananchi wamekuwa wakiishauri Nec kuahirisha Kura ya Maoni huku vyama vya siasa vikimtaka Rais Jakaya Kikwete atii makubaliano yaliyofikiwa na Kituo cha Demokrasia (TCD) mwaka jana ya kuahirisha zoezi hilo hadi baada ya Uchaguzi mkuu.
Jaji Lubuva alisema kuwa tume yake inaendelea kuboresha daftari la wapiga kura nchi nzima ambapo wanatarajia kukamilisha ifikapo Julai mwaka huu. Nec ilieleza kuwa baada ya kumaliza uandikishaji mkoani Njombe watahamia mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara na Iringa.
MWANANCHI
Mwanamke mmoja aliyejeruhiwa na wananchi ametelekezwa barabarani na wauguzi wa Zahanati ya Nzera iliyopo Geita kwa kile kinachodaiwa ni mchawi.
Hata hivyo kaimu mganga wa Zahanati hiyo Bigaeli Kasala alipinga madai hayo akisema hajatelekezwa bali bali alikuwa akitafutiwa usafiri wa kumpeleka Geita kwa matibabu zaidi.
“Huyu mgonjwa hatujamtupa,niliwakabidhi wahusumu wampandishe basi la asubuhi linalokwenda Geita lakini inaonekana walipitwa na basi hivyo wakamuacha barabarani akisubiri basi jingine”–Kasala.
Dk. Kasala alisema kituo chao hakina gari la wagonjwa ndio maana walimwacha barabarani akisubiri gari lingine.
Awali alidai mwanamke huyo alipelekwa Zahanati hapo wa kituo ch polisi baada ya kumwokoa mikononi mwa wananchi waliokuwa wakimpiga wakimtuhumu kuwa ni mchawi.
Alisema alikutwa kwenye nyumba akiwa mtupu na kutuhumiwa alikuwa akifanya uchawi na ndipo watu wakaanza kumpiga hadi kumvunja kiuno.
MWANANCHI
Hoja 22 za kupinga vifungu Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015 zilizotolewa juzi na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana zilisababisha kikao cha 14 cha Bunge kuvunja rekodi ya kutumia muda mrefu baada ya kumalizika saa 6.15 usiku.
Marekebisho yaliyowasilishwa na Lissu yaliungwa mkono na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye pia alikuwa na marekebisho yake katika muswada huo, hivyo wote wawili kuichachafya Serikali bila mafanikio baada ya muswada huo kupitishwa kwa sauti kubwa ya “Ndiyooo” ya wabunge wa CCM.
Kuanzia saa 12.30 jioni, Bunge lilikaa kama kamati kupitisha muswada huo baada ya kumaliza kuupitisha muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ambao haukuwa na mvutano mkali.
Mvutano wa kisheria kati ya Lissu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, naibu wake, January Makamba ulianza saa 12.30 jioni hadi saa 5.30 usiku na baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akatumia muda uliosalia kuahirisha Bunge.
Mpaka inafika saa 5.00 usiku wabunge wa upinzani waliokuwapo bungeni walikuwa 12 tu, akiwamo Lissu na Mnyika na hivyo kufanya idadi ya wabunge wote kuwa 86, wakiwamo wa CCM na mawaziri.
Kuna wakati Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alilazimika kusimama kutoa ufafanuzi wa kina, ikiwa ni pamoja na namna ya kuvitamka kwa ufasaha vifungu vya sheria ili kukubalika na pande mbili zilizokuwa zinavutana.
Mapendekezo yote yaliyotolewa na Chenge ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaliungwa mkono na Lissu pamoja na Masaju na Wizara ya Mawasiliano.
Wakati mnyukano huo ukiendelea, Pinda alikuwa kimya akisubiri kusoma hotuba yake ya kuahirisha Bunge.
Pinda alianza kusoma hotuba hiyo saa 5.30 usiku mpaka saa 6.00 usiku, ikiwa ni baada ya Bunge kuupitisha muswada huo. Baada ya dakika 15 za kutoa matangazo mbalimbali na kuwashukuru wabunge, Spika Makinda aliahirisha mkutano huo.
Kuna wakati Lissu aliwataka wabunge kutochoka kutokana na hoja anazozitoa kusababisha kikao hicho kuwa kirefu, huku Makinda naye akiwaeleza wabunge kuwa ‘zege halilali’, akimaanisha kuwa Bunge haliwezi kuahirishwa mpaka muswada huo upitishwe na Pinda atoe hotuba ya kuahirisha Bunge.
Kati ya marekebisho 22 yaliyowasilishwa na Lissu, ni matano tu yaliyokubaliwa na Serikali huku Lissu akikubali vifungu viwili tu vilivyofanyiwa marekebisho na Serikali, akivisifia kuwa vimeandikwa kama sheria inavyotaka, lakini vingine akiviita vya ovyo na sheria inayotungwa ni mbaya yenye malengo ya kuwakomoa baadhi ya watu.
MWANANCHI
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Ziwa Magharibi, kimeanzisha operesheni maalumu kwa ajili ya kusaka ubunge katika majimbo yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ambayo yanashikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Operesheni hiyo inayojulikana kama ‘tigitigi’, ilianza juzi kwa kutumia usafiri wa helikopta katika majimbo kadhaa, ikiwamo Jimbo la Sengerema linaloshikiliwa na mbunge wa sasa, William Ngeleja.
Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo ni miongoni mwa makada wa chama hicho waliofika katika jimbo la Sengerema juzi, wakiambatana na kada wa chama hicho anayetaka kutangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo, Hamis Tabasamu.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji tofauti kwa muda wa dakika 30 katika kila kijiji, Mawazo alisema wameanzisha operesheni hiyo kwa lengo la kushinda ubunge kwenye majimbo yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ili kuleta ukombozi wa kweli kwa wananchi.
“Wananchi naomba niwambie tumeanza na Jimbo la Sengerema, tutapambana hadi hatua ya mwisho ili kulikomboa jimbo hili. Tunataka Kanda ya Ziwa iwe ya mfano, tutazunguka kata zote na vijiji vyote katika mikoa ya Geita, Simiyu, Mwanza, Tabora, Shinyanga na Mara kuelimisha wananchi,” alisema Mawazo na kuongeza’
“Pia naomba wananchi mjitokeze kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili tuweze kupata nafasi ya kufanya mabadiliko ya kweli mwezi Oktoba. Ndugu zangu mapambano yameanza hakuna kulala, huu ni wakati wetu Chadema,” alisema.
Naye mtangaza nia wa jimbo hilo, Hamis Tabasamu ambaye aliwahi kuwa diwani wa Sengerema, alisema kuwa watafungua ofisi 78 za Chadema kwenye jimbo hilo ili wananchi waweze kuwa na sehemu za kutoa malalamiko yao kwa viongozi na kuhudumiwa.
Alisema muda uliopo sasa ni wa kufanya mabadiliko na kwamba kazi ya kutafuta ukombozi Sengerema imeanza, hivyo ni jukumu la wananchi wa eneo kuunga mkono jitihada za chama hicho za kuwaletea maendeleo endelevu.
MTANZANIA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Taasisi ya Taaluma na Maendeleo, Dk. Stephen Maluka, ametangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Nyasa (Mbinga Magharibi) mkoani Ruvuma kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Oktoba mwaka huu.
Dk. Maluka mwenye Shahada ya Uzamivu ya Afya ya Jamii aliyopata nchini Sweden, amejitosa kugombea jimbo hilo ambalo awali lilijulikana kama Mbinga Magharibi na lilikuwa likiongozwa na marehemu Kapteni John Komba ambaye alifariki mwanzoni mwa mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Dk. Maluka alisema lengo la kuingia katika kinyang’anyiro hicho ni kuwakomboa wananchi wa jimbo hilo, ambao kwa sasa wana hali ngumu ambayo ilichangiwa na usimamizi mbovu wa rasilimali na bajeti za Serikali.
Alisema upungufu uliopo katika jimbo hilo ni wa kiuongozi na endapo kutatokea mtu atakayekuwa na usimamizi mzuri katika masuala muhimu atakuwa na nafasi nzuri ya kubadilisha maisha ya wananchi waliopo.
“Nalijua Jimbo la Nyasa matatizo yote yanatokana na usimamizi mbovu wa viongozi katika miradi ya Serikali na fedha za bajeti zinazotolewa kwa ajili ya jimbo hilo.
Alisema endapo atapata nafasi hiyo atasimamia kwa umakini mapato na matumizi ya jimbo ili kuhakikisha yanamnufaisha kila mwananchi.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia watu saba wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa vituo vitatu vilivyogundulika kuhifadhi watoto 147 kwa siri Katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alitoa taarifa hiyo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kwamba, watu hao wanashikiliwa kwa kosa la kulea watoto katika mazingira hatarishi na kusababisha wengine wasiendelee na masomo kinyume cha sheria.
“Tunawashikilia watu saba ambao inasemekana ni wamiliki wa vituo hivyo kwa tuhuma za kuwahifadhi watoto kinyume cha sheria.
“Katika Msikiti wa Bilal tumekamata watuhumiwa wawili, katika Msikiti wa Othman tumekamata watuhumiwa wawili na katika Msikiti wa Kwa Kiriwe Markes bin Kain, tumekamata watuhumiwa watatu,” Kamanda Kamwela.
Akifafanua zaidi, Kamanda Kamwela alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuna mtandao wa walimu wengi wanaofundisha watoto hao.
Katika hatua nyingine, kamanda huyo wa polisi, alitoa wito kwa wananchi mkoani hapa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kufichua wahalifu, wakiwamo wanaolea watoto bila kufuata utaratibu.
Watoto wa kiume wenye umri kati ya miaka 11 na 21 kutoka mikoa mbalimbali nchini walikutwa juzi wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, wakilelewa misikitini.
Kugundulika kwa watoto hao ni mwendelezo wa matukio ya watoto kukamatwa mkoani hapa baada ya watoto wengine 30 kugunduliwa mwezi uliopita katika maeneo mawili tofauti.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza>>>twitter Insta Facebook