Premier Bet
TMDA Ad

Magazeti

Stori 9 zilizopewa headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania Februari 12, 2015 ziko hapa

on

blllMWANANCHI

Matukio ya wasafiri kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa na nyara za Serikali na dawa za kulevya, yanazidi kuchukua sura mpya baada ya raia mmoja wa Ubelgiji kukamatwa akiwa na fuvu la binadamu.

Raia huyo, Balcjan Christine Weejktgns (49) alikamatwa Jumatatu saa 2:30 usiku wakati akiwa katika taratibu za kuingia uwanjani hapo tayari kwa safari ya kuelekea Ubelgiji kupitia Zurich, Uswisi.

Tukio la kukamatwa kwa Mbelgiji huyo ni mwendelezo wa matukio ya aina yake uwanjani hapo baada ya watu wengine wawili kukamatwa kwa nyakati tofauti kwenye uwanja huo wakiwa na kucha za simba na kenge walio hai.

Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege, Hamisi Selemani alisema mtu huyo alikutwa ameficha fuvu hilo la binadamu kwenye mfuko wa plastiki.

Alivyopita kwenye mashine za ukaguzi tulimtilia shaka na tulipompekua tulimkuta amebeba fuvu la kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa plastiki ndani ya sanduku alimokuwa ameweka nguo zake na vitu mbalimbali:-Selemani.

Raia huyo anadaiwa kuwa ni mkazi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro na inadaiwa kuwa alikuwa nchini kwa ajili ya kufanya utafiti.

MWANANCHI

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekiri kuwapo kwa baadhi ya watumishi wake wanaojihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, hivyo kuchafua sifa ya taasisi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na taasisi zilizofanya utafiti juu ya masuala ya rushwa nchini, baadhi yake zina ukweli.

Dk Hoseah alisema wanapokea utafiti huo kama changamoto na watatumia sheria, kanuni na taratibu kuwapa adhabu watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Takukuru siyo malaika, iwapo nitasema hakuna kabisa rushwa ndani ya taasisi hii nitakuwa ninajidanganya kwani hili tatizo lipo sehemu zote, inawezekana maofisa wasio waadilifu wanapokea rushwa lakini ninawahakikishia kwamba tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika:Dk Hoseah 

Pia, alitoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na matapeli wanaojitangaza kwamba wao ni maofisa wa Takukuru, hivyo kuomba rushwa kwa baadhi ya maofisa wa Serikali na watu wengine ambao wanabainika kufanya makosa yanayohusiana na ubadhirifu mbalimbali.

MWANANCHI

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro amesema kila kata nchini itapata nakala 300 za Katiba Inayopendekezwa ili kuwawezesha wananchi  kuisoma na kushiriki katika Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu.

Amesema mpaka kufikia Februari 9, mikoa 11 nchini ilikuwa tayari imepatiwa nakala hizo na kwamba Serikali imepanga kuchapisha nakala milioni 2 kwa ajili ya kuzisambaza nchi nzima.

Amesema nchini kuna zaidi kata 3,800 na lengo la Serikali ni kusambaza nakala hizo kwenye vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na majiji.

Dk Migiro alisema mbali na nakala hizo, Katiba Inayopendekezwa pia imewekwa katika tovuti za Wizara ya Katiba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bunge.

Wananchi waliokuwa katika miji na vijiji siyo wote wanaweza kupata nakala katika mtandao. Ukiwa na  nakala halisi unaisoma wakati wote kwa hiyo Serikali imekuwa na nia ya kuwapatia watanzania nakala halisi haraka iwezekanavyo:Migiro

MWANANCHI

Klabu ya Simba imewapa masharti mahasimu wao wa jadi, Yanga kama inahitaji mashabiki wao waishangilie kwenye mchezo wa keshokutwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), dhidi ya BDF IX ya Botswana.

Simba ilieleza jana kuwa katika mchezo huo, mashabiki wake wataingia uwanjani wakitanguliza utaifa kwanza, lakini kwa sharti la Yanga kutowaangusha na kucheza mpira wenye kiwango, kinyume na hapo watabadilika na kuelekeza nguvu zao kwa wapinzani, BDF.

Rais wa Simba, Evance Aveva alisema kuwa katika mchezo huo watakuwa upande wa Yanga iwapo watacheza mpira wenye kiwango kama ule unaochezwa nao (Simba), tofauti na hivyo watawageuka katikati ya mchezo.

Kwenye mechi hiyo tutatanguliza utaifa kwanza kwa kuiunga mkono Yanga mwanzoni mwa mchezo na tutaendelea kufanya hivyo hadi mwisho, kinyume chake tutawageuka.

Ingawa haijawahi kutokea Simba ikaishangilia Yanga, lakini kwenye mchezo huu tumeamua kutanguliza mbele utaifa, lakini tukiona Yanga ‘wanambwelambwela’ (hawaeleweki) uwanjani kwa kucheza chini ya kiwango tutawabadilikia na tutaiunga mkono BDF:-Aveva.

NIPASHE

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), inatarajia kuanzisha kitengo cha magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya kubeba wagonjwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Jiji.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi wa MNH, Dk. Hussein Kidanto, wakati wakisaini makubaliano ya kupokea msaada wa magari mawili ya kubebea wagonjwa kutoka kwa Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada.

Dk. Kidanto, alisema kwa sasa hospitali hiyo ina gari moja la wagonjwa ambalo linashindwa kukusanya wagonjwa na kuwapeleka katika hospitali hiyo na chini ya kitengo hicho wataanza na magari 10.

Tunaushukuru Ubalozi wa Japan kwa kutoa msaada huu, utakuwa mwanzo wa kuanzisha kitengo cha huduma ya magari ya wagonjwa ambacho tunakianzisha Muhimbili ili yaweze kuwabeba kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji:Dk. Kidanto.

Alifafanua kuwa, magari hayo yataandikwa namba maalum za maeneo tofauti ya Jiji na yatabeba watu watakaopatwa na ugonjwa wa ghafla kama mama wajawazito, wenye magonjwa ya moyo na maengine kwa lengo la kuwafikisha hospitali wakiwa salama.

NIPASHE

Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Tanga, kimevunjika mara tatu mfululizo kutokana na madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kufanyiana vurugu na kukunjana kutaka kuzichapa kavu kavu.

Vurugu hizo zimetokana na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuendelea kumtambua na kumwita katika vikao vya Baraza la Madiwani wa jiji hilo aliyekuwa Diwani wa Kata ya Malungu (CUF), Mohamed Mwambeya, wakati alishajiondoa katika chama hicho.

Mwambeya ambaye alipata udiwani wa kata hiyo kupitia CUF,  Agosti, mwaka jana, alitangaza kukihama chama hicho na kuhamia CCM wakati wa mkutano wa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdallah Bulembo alipofanya ziara mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, nafasi zote za kuchaguliwa za kisiasa kwa maana ya rais, ubunge na diwani, ni lazima atokane na chama cha siasa na masharti hayo pia yapo katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Hivyo kutokana na katiba hiyo, Mwambeya ambaye alitangaza kujiondoa CUF na kujiunga CCM  ni wazi kuwa udiwani wake utakuwa umekoma na msimamizi wa uchaguzi alistahili kutangaza kuwa kata hiyo ipo wazi ili kufanyike mchakato wa kuchagua diwani mwingine atakayetokana na chama cha siasa.

MTANZANIA

Hatimaye mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Emmanuel Mbasha, ameibuka na kuweka wazi suala la mgogoro wa mtoto na mkewe Flora Mbasha.

Hatua hiyo imekuja miezi saba tangu wawili hao walipoingia katika mgogoro wa ndoa yao hali iliyosababisha Mbasha kufikishwa mahakamani kwa kosa la ubakaji.

Hivi karibuni, picha za mtoto mchanga zilisambazwa katika mitandao ya kijamii na kudaiwa kuwa ni wa Flora aliyezaa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kuahirishwa kwa kesi ya ubakaji inayomkabili katika Mahakama ya Ilala, Mbasha alisema hayupo tayari kuzungumzia kuzaliwa kwa mtoto huyo, ila anayeweza kueleza ukweli kuhusu baba wa mtoto ni Flora mwenyewe.

Siwezi kuongea chochote, ukweli wote anaujua Flora nendeni mkamfuate atawaeleza, na sijaongea na gazeti lolote kuhusu mtoto huyo… kwa sasa sipo tayari kusema lolote:- Mbasha.

HABARILEO

BAADA ya kushuka kwa bei ya mafuta nchini, wakati wowote kuanzia leo Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) linatarajiwa kutangaza bei mpya za umeme ambazo zitakuwa na unafuu kwa wananchi.

Kutangazwa kwa bei hiyo ni agizo la Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene la kuwataka kuangalia uwezekano wa kushusha gharama za umeme ili kushuka kwa mafuta kuwaguse moja kwa moja wananchi wa kawaida.

Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) nayo imetakiwa kuangalia namna itakavyoweza kushusha bei za nauli ili kushuka kwa gharama za mafuta, kuendane sambamba na kuwagusa wananchi.

Simbachawene alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, baada ya mkutano wa pamoja kati ya wadau na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na wizara hiyo.

Alisema, ingawa matumizi ya mafuta katika kuzalisha umeme yamepungua, lakini kwa mitambo na kiasi kinachotumika katika kuzalisha umeme lazima ionekane kushuka kwa bei ya umeme.

Tanesco waangalie ni kwa kiasi gani gharama za uzalishaji, kwa sababu hizo gharama za uzalishaji wa umeme ndiyo zinazotumika kupanga bei ya umeme. ”Hivyo lazima tuoneshe Ewura ‘

HABARILEO

Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Urassa amefutiwa mashitaka ya kupokea sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kusomewa mashitaka ya kupokea rushwa ya Sh milioni 161.7.

Urassa aliondolewa mashitaka hayo jana baada ya Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kubadilisha hati ya mashitaka dhidi yake.

Akisoma hati hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda, Swai alidai Februari 14, 2014 katika eneo la Benki ya Mkombozi, Urassa akiwa Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco alipokea rushwa ya Sh 161,700,000 kupitia akaunti namba 00120102658101.

Alidai Urassa alipokea fedha hizo kutoka kwa Mshauri wa Kimataifa ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering na Mkurugenzi wa zamani wa IPTL, James Rugemalira kama tuzo hiyo baada ya kuiwakilisha Tanesco na IPTL katika kesi ya Standard Charter nchini Hong Kong.

Upelelezi wa kesi umekamilika lakini upande wa utetezi ulidai kuna masuala ya kikatiba yanajitokeza katika kesi hiyo ambayo yanatakiwa kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook

Tupia Comments