NIPASHE
Askari Polisi PC Joseph Swai, ameuawa wakati akimwokoa mtoto wa miezi minane, aliyekuwa akiteswa na baba yake mzazi katika mtaa wa Chang’ombe Juu mjini hapa.
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 5:00 asubuhi na kumtaja mtoto aliyekuwa anateswa kuwa ni Valerian Mallya.
Alisema awali, polisi huyo alipigiwa simu na Mtendaji wa mtaa wa Chang’ombe Juu, akimjulisha kuwa amepokea taarifa kutoka kwa Oliva Baltazar (52), kuwa kijana wake, Tisi Mallya (29), anamtesa mtoto wake.
Alisema polisi huyo alikwenda eneo la tukio na alipofika aligonga mlango huku akijitambulisha kuwa ni askari, kisha akamuamuru atoke nje.
Hata hivyo, alisema Mallya alimnyanyua mtoto wake huyo kwa mkono mmoja miguu ikiwa juu na kichwa chini, akitishia kumuua kwa panga.
Kamanda Misime alisema askari huyo aliamua kumwokoa mtoto huyo kwa kumrukia mtuhumiwa lakini aliteleza na kuanguka chini na ndipo mtuhumiwa huyo alipopata mwanya wa kumkata kichwani na maeneo mengine ya mwili.
NIPASHE
Ni simanzi na majonzi katika kijiji cha Ndami, wilayani Kwimba ikiwa ni siku 40 sasa, tangu mtoto Pendo Emmanuel (4), atekwe na watu ambao hawajajulikana hadi sasa.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mwandu Madirisha, anasema wananchi wake hawapo vizuri kiakili tangu aibwe mtoto Pendo na kwamba “hawaamini kama mtoto yule hajaonekana mpaka leo.”
Anasema kijiji hicho kina barabara kuu tatu zinazoingia na kutoka katika vitongoji vya Misasi, Nyahonge na Chibwiji, hali inayochangia kuwapo na ulinzi wa jadi (sungusungu).
Pendo, hakuna aliyefahamu wala kuhisi chochote kwani tumezoea kuishi kwa amani kwa miaka mingi,” anasema.
Mwenyekiti huyo anasema inawezekana watu hao walitumia hali hiyo kufanya ‘uhalifu’ wa kuvamia nyumba yao iliyopo mbali kidogo na barabara zinazolindwa na sungusungu.
“Naamini ni tukio la imani za kishirikina linalowahusu zaidi wafanyabiashara wa migodini pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ambao wanahitaji madaraka,” anasema.
Mama mzazi wa Pendo, Sophia Juma, ambaye kwa sasa amehamishwa katika makazi yake na kupelekwa wilayani Misungwi, hakuwa na mengi ya kusema kutokana na kumfikiria mtoto wake.
“Namkumbuka sana mwanangu, sielewi huko alipo kipi kimemtokea, lakini namwamini Mungu waliotenda jambo hilo, uso wa Mungu utawaumbua:-Sophia.
NIPASHE
Wanafunzi wawili wa darasa la nne katika shule ya msingi ya Unity, iliyopo Chamazi, eneo la Mbagala, Manispaa ya Temeke, wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa darasa la shule hiyo uliogongwa na gari.
Kadhalika, wanafunzi watatu wamejeruhiwa baada ya kijana wa kazi wa mmiliki wa shule hiyo, ambaye siyo dereva kujaribu kuendesha gari na kuparamia darasa hilo na sehemu ya ukuta kuwaangukia wanafunzi waliokuwa darasani wakiendelea na masomo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kihenya Kihenya, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea Februari 03, mwaka huu, majira ya saa 2:30 asubuhi, na wanafunzi wawili wamefariki na watatu kujeruhiwa na kwamba mtuhumiwa wa tukio hilo anashikiliwa na jeshi la Polisi.
“Wanafunzi watatu wametibiwa katika hospitali ya Mbagala na wameruhisiwa baada ya kupata nafuu,” alisema.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema chanzo cha ukuta huo kuanguka ni kijana mmoja wa familia hiyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30, ambaye ni mmoja wa wanafamilia ya nyumba hiyo, aliyeendesha gari aina ya Rav 4 ambalo liliparamia ukuta huo.
“Tulijiuliza nini kilitokea na baadaye tulimuona kijana aliyeendesha gari akiwa ndani ya gari, tulimtoa akiwa hajitambui na gari imeharibika vibaya, tulimpepea hadi akazinguka, tuliwajulisha polisi na baadaye kupelekwa kituo kikuu cha polisi cha Kizuiani,”.
MWANANCHI
Dar es Salaam.Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka viongozi wa dini kutumia nafasi kukemea juu ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa waumini wao na kuelimisha madhara yanayoweza kusababishwa na teknolojia hiyo katika jamii.
Hatua hiyo ya TCRA imekuja kufuatia kukithiri kwa vitendo vinavyoashiria kutumika vibaya kwa mitandao ya kijamii kama njia ya mawasiliano hali inayochangia kuzidi kuporomoka kwa maadili.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Prof. John Nkoma alisema lengo la kukutana na viongozi hao ni kuwapa elimu kuhusiana na madhara ambayo jamii inaweza kupata kufuatia ongezeko la matumizi mabaya ya mitandao.
“Mitandao ni mizuri sana lakini tatizo ni jinsi inavyotumika watu wamekuwa wakifanya mambo ya ajabu tena bila kuwa na hofu ya Mungu ndiyo maana tumerudi kwenu viongozi wa dini mtusaidie katika hili:-Nkoma
Kwa kutumia nafasi zenu tuna imani mtawaelimisha waumini ili waelewe kuwa kusambaza ujumbe unaoashiria uchochezi ni kosa kisheria na inaweza kuwa dhambi kwani hakuna ambaye angependa amani ivunjike”
MWANANCHI
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imetoa siku 80 kwa uongozi wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) kuhakikisha kinafanya uchaguzi wake wa ndani wa kuwapata viongozi wapya.
Kauli hiyo imeitolewa baada ya baadhi ya wanachama wa chama hicho kufikisha malalamiko katika ofisi hiyo wakiiomba itangaze kwamba uongozi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema umefikia kikomo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukweli na Maridhiano wa TLP Taifa, Joram Kinanda alimtuhumu Mrema kukiuka katiba ya chama hicho, kuongoza chama kidikteta, kuporomosha heshima ya chama na kujilimbikizia madaraka.
MTANZANIA
SIKU chache baada ya picha za mtoto mchanga kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kudai kuwa ni za mtoto wa mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Flora Mbasha kuwa amezaa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima hatimaye wawili hao wamefunguka.
Hatua hiyo imekuja miezi saba tangu wawili hao walipoingia katika mgogoro wa ndoa yao hali iliyosababisha mume wa Flora, Emmanuel Mbasha kufikishwa mahakamani kwa kosa la ubakaji.
Mchungaji Gwajima, alisema taarifa hizo ni za uzushi na huenda zinasambazwa na mume wa Flora.
Mchungaji Gwajima alikwenda mbali na kusema pamoja na uzushi huo unaosambazwa dhidi yake kwa kuhusishwa katika uhusiano na Flora anamwachia Mungu kila kitu.
“Hahaha… si unajua hiyo issue (suala, jambo) ya Mbasha ni ya muda mrefu tu… wakati mwingine mimi huwa sijibu ujinga,” alisema Gwajima huku akicheka.
“Awali niliwaza kuwashitaki (alipoanza kuhusishwa kwamba ana uhusiano na Flora) wanaoeneza uzushi huo lakini nikaona ‘It doesn’t hold water’ (haina mashiko), najua shutuma hizo zinatoka wapi:-Gwajima.
“Mimi sikujua kama alikuwa mjamzito, hata taarifa kwamba amejifungua ndiyo nazisikia kwako. Hapa nimetoka ‘airport’, sikuwepo Dar es Salaam.
Flora akizungumza kwa njia ya simu alisema “Siko tayari kuzungumza lolote kuhusu Mbasha kwa sasa. Yeye anajeuri ya pesa ndo maana anafanya haya yote lakini mimi ninasimama na Mungu wangu na ninajua Mungu atanipigania:-Flora.
MTANZANIA
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kupanda kizimbani katika mahakama ya Afrika Mashariki EAJC kutoa ushahidi dhidi ya kesi ya kukiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Watanzania Ally Msangi,David Makata na John Adam akipinga hatua ya Serikali za Kenya,Uganda na Rwanda kufanya vikao vitatu mfululizo vya maendeleo ya nchi zao na kuitenga Tanzania na Burundi.
Taarifa zilizopatikana jiji hapa jana na kuthibitishwa na wakili mwandamizi wa walalamikaji katika kesi hiyo Jimy Obedi alisema mbali ya ushahidi wa walalamikaji,wanatarajia shahidi atakua Tais Kikwete.
Alisema hatua ya awali ya usikilizaji imekamilika na kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa February 24.
“Usikilizwaji wa awali mara nyingi ni kuangalia mpangilio wa kesi,namna ya orodha ya mashahidi wetu na mambo mengine ya kisheria,sasa hayo tumeyakamilisha:-Obedi
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook