MWANANCHI
Watu 42 wamepoteza maisha na wengine 23 kujeruhiwa baada ya lori la mizigo kugongana na basi na kontena lililokuwa limebebwa kuangukia gari hilo la abiria, katika ajali ya aina yake iliyotokea eneo la Mafinga Changalawe mkoani Iringa.
Watu 37 waliokuwa kwenye basi hilo la kampuni ya Majinjah Express lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam, walifariki papo hapo na wengine watano kufariki wakiwa Hospitali ya Mafinga. Dereva wa basi na wa lori hilo la kampuni ya Cipex, pia wamefariki.
Shuhuda mmoja wa ajali hiyo, Nyasio Pascal, aliyekuwa akiendesha basi la Saibaba, alisema aliliona lori hilo likijaribu kukwepa mashimo kwenye barabara hiyo ambayo ni nyembamba, na mara likaanza kuyumba kulia na kushoto baada ya kukanyaga shimo na ndipo lilipolifuata basi na kugongana nalo.
Alisema kontena lililokuwa limebebwa na lori hilo, liliangukia juu ya basi na kulikandamiza, jambo ambalo lilisababisha vifo vya watu wengi na pia kuzuia watu waliokuwa karibu na ajali kuokoa watu waliojeruhiwa hadi tingatinga lilipowasili. Hata hivyo, alisema mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja, alinusurika kwenye ajali hiyo bila ya kudhurika.
Miili ya waliokufa imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mafinga, ambayo ina chumba cha kuhifadhia miili ya watu saba tu, na mingine imepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa.
“Hii ni ajali mbaya ambayo haijawahi kutokea mkoani hapa,” alisema mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyefika eneo hilo la ajali.
NIPASHE
Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Zitto amesema hajapewa taarifa rasmi, hivyo ataendelea kuwa mbunge.
Pamoja na kauli hiyo ya Zitto, viongozi wa Chadema wamesema hawatahangaika kumwandikia barua kumjulisha hatua zilizochukuliwa na chama hicho dhidi yake.
Zitto akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, alisema ataendelea na kazi yake ya ubunge kwasababu hajapewa taarifa rasmi na Chadema kuhusu uamuzi uliochukuliwa wa kumvua uanachama.
“Sina taarifa rasmi kilichotokea na kama mnavyoona naendelea na vikao vya kamati kama kawaida na leo (jana) nitakuwa na watu wa Benki Kuu (BoT), TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Ijumaa nitakwenda Kigoma jimboni kwangu kwa ajili ya kazi zangu, niliwahidi wananchi wangu nitakwenda kabla ya kwenda bungeni, kimsingi mimi bado ni mbunge,” Zitto.
Licha ya Chadema kutangaza kumvua uanachama, Zitto jana aliendesha vikao vya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kama kawaida.
Zitto alisema hawezi kujibishana na chama chake kwani hajalelewa katika maadili kama hayo na kwamba kitu muhimu kwake ni kazi ya kuwatumikia Watanzania.
“Mimi huwezi ukanilinganisha na mbunge yeyote katika kazi ambazo nimekuwa nikizifanya, siasa kwangu ni ‘issues’ tofauti na watu wengine ambao siasa zao ni kugombana na watu, kwangu hizi ni changamoto, nakomazwa,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema chama hicho hakitahangaika kumwandikia barua Zitto kumjulisha uamuzi wake kwa kuwa anajua alishakiuka Katiba ya chama kwa kushtaki hivyo uanachama wake unakoma mara moja.
NIPASHE
Kundi jipya la kihalifu linalojulikana kwa jina la Libya limeibuka jijini la Dar es Salaam na kuvamia eneo la kituo cha daladala cha Tabata Mawenzi na kufanya uharibifu mkubwa uliosababisha magari kadhaa kuvunjwa vioo na kuzua taharuki kubwa miongoni mwa wakazi, wafanyabiashara na wapita njia katika eneo hilo.
Kundi hilo limeibuka ikiwa ni miezi chache baada ya kundi la vijana wa kihalifu, maarufu kama ‘Panya Road’ kufanya vurugu na kuzusha hofu kubwa jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea jana na vijana wawili wametiwa mbaroni na hadi tunakwenda mitamboni walikuwa wakiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Mary Nzuki, alithibitisha kutokea vurugu hizo.
Vurugu hizo zilizuka juzi majira ya saa 8 mchana baada ya vijana hao kutoka kwenye mazishi ya mwenzao anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira.
Kijana huyo, Amiri Shabani (14-15), maarufu kwa jina la “Ega”, ambaye ni mkazi wa maeneo ya mtaa wa Twiga, kata ya Kimanga, anadaiwa kuuawa usiku wa kuamkia juzi.
Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa, kijana huyo aliuawa kwa kupigwa na wananchi hao baada ya kumvamia njiani mwanamke aliyekuwa akipita eneo la Mawenzi na kujaribu kumpora mkoba wake, ambao ndani yake kulikuwa na fedha.
NIPASHE
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi kubaini zilikopotelea Sh. milioni 699 zilizotolewa na Wizara ya Fedha kwenda Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambazo hazijulikani ziliko sasa.
Aidha, PAC imeagiza Tanesco kuwasilisha katika ofisi ya Bunge mikataba yote ya kampuni zinazozalisha umeme nchini ambazo zimeingia nayo mikataba ili kupitiwa upya na kuwa kumbukumbu kwa Bunge.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alitoa maelekezo hayo jana katika kikao baina ya kamati hiyo na menejimenti ya Tanesco na kusema kumekuwa na mvutano kuhusu Sh. milioni 699 zilizotolewa na Hazina kwenda Tanesco.
Zitto alisema inawezekana fedha hizo zimetolewa kwa Tanesco, lakini zimetumika vibaya au Hazina wamezitoa kwa mtu tofauti, hali ambayo imekuwa ikileta mkanganyiko ambao unahitaji kufanyiwa uchunguzi.
Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha Tanesco, Anetha Chegula, alisema fedha hizo zinadaiwa kutolewa na Hazina tangu mwaka 2012 kwenda Tanesco kwa ajili ya kusaidia miradi ya umeme, lakini hazijafika katika shirika hilo licha ya Hazina kuonyesha kuwa zilishatolewa.
Chengula alisema wamekuwa wakiitaka Hazina kuonyesha vielelezo vinavyoonyesha kuwa fedha hizo zimepelekwa Tanesco, lakini hadi mwaka jana Hazina haikufanya hivyo huku Tanesco ikifanya uchunguzi katika akaunti zake bila kuziona fedha hizo.
Akizungumzia mikataba ya makampuni ya Agrecco, Symbion, Songas na IPTL , alisema ipelekwe haraka ofisi za Katibu wa Bunge ili iwe kumbukumbu kwa Bunge.
Wabunge walisema tozo ya uendeshaji wa mitambo (capacity charge) iangaliwe upya kwa sababu inaingiza gharama kubwa kwa Tanesco, hivyo kushindwa kufikia malengo ya kujiendesha badala yake kuendelea kutegemea serikali kulisaidia.
Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy, alisema ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini ni kwa Tanesco kuchukua hatua ya kuinunua mitambo ya umeme inayomilikiwa na kampuni zinazozalisha umeme na kuiuzia Tanesco kwa bei ya juu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema Songas inalipwa Sh. bilioni 8.562 za tozo ya uendeshaji, IPTL Sh. bilioni 4.302 na Aggrecco Sh. bilioni 1.600 kwa mwezi. Mramba alisema Aggreco imekuwa ikiiuzia Tanesco umeme kwa Dola za Marekani senti 40 na IPTL senti 23 huku Tanesco ikiuza umeme huo kwa senti Dola za Marekani 26.
NIPASHE
Serikali imesema asilimia tano kati ya 17 inayochangiwa na wahisani wa maendeleo katika bajeti ya mwaka huu imeathirika kutokana na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya mkutano kati ya serikali, wadau na wahisani wa maendeleo kwa nchi zinazoendelea.
Lengo la mkutano huo ni kufanya majadiliano ili kufahamu mwenendo mzima wa bajeti ya serikali ulipofikia na maeneo yanayohitaji kurekebishwa.
Mkuya alisema kutokana na sakata la Escrow lililojitokeza baada ya bajeti kupitishwa, wameona ipo haja ya kuangalia upya mfumo mzima na mikakati yao ya utekelezaji wa bajeti hiyo ili kujua kama bado itaendelea kuwa hai katika utekelezaji wake.
“Katika hili tumeona upo umuhimu wa kutazama upya makubalianao na misingi yetu kama imepoteza uhalisia kiutendaji au la ili kujua tutaendeleaje nayo hata baada ya kujitokeza kwa jambo hili,” Mkuya.
Aliongeza kuwa kutokana na hatua stahiki na za wazi zilizochukuliwa na serikali, wahisani wameridhika na wataendelea na utekelezaji wa kuchangia bajeti hiyo kama walivyokubaliana.
“Si vyema bajeti ya serikali iathirike kutokana na mambo yanayojitokeza, na hivi sasa fedha tutakazopata tutazielekeza katika maeneo ya barabara, maji na nishati kama ilivyopendekezwa,” alisema.
Alisema wiki mbili kuanzia sasa takribani Dola milioni 44 (zaidi ya Sh. bilioni 50) huku Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika wakijipanga kutoa Dola millioni 227 (Sh. bilioni 409).
Alisema nchi zinazoendelea zinakabiliwa na masharti magumu katika kupewa misaada, hivyo uwapo utaratibu maalum wa upokeaji wa misaada ili kuepusha kukwama pindi matatizo yanapojitokeza baada ya makubalinao na wahisani.
NIPASHE
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekanusha tuhuma za kuwahusisha baadhi ya viongozi wake waandamizi kuwa wanapanga njama za kumdhuru Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, kikisema ni za uongo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema tuhuma hizo ni za kipuuzi na uongo, lakini zisipojibiwa zinaweza kugeuka ajenda.
Alisema ni vizuri Watanzania wakakumbuka historia ya tuhuma lukuki zilizowahi kutolewa na Dk. Slaa tangu aanze siasa na zote zilithibitika baadaye kuwa ni za uongo. “Kupanga kumdhuru Dk. Slaa, ili CCM ipate nini kwa kudhurika kwake.
“Kwa nini CCM ipange kumdhuru, huu ni mwendelezo wa tabia yake ya kuzusha mambo ya uongo kila anapoona anachuja kisiasa, ni busara kwa umri wake akatumia muda mwingi kumrudia Mwenyezi Mungu,” Nape.
Alitaja mambo ambayo Dk. Slaa amewahi kuzusha kuwa ni pamoja na kuwatangazia wananchi wakati wa kampeni za mwaka 2010, akiwa mkoani Singida kuwa wananchi kwamba lilikamatwa lori la mizigo lililojazwa karatasi za kura za urais zilizokuwa tayari amepigiwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
“Katika kuonyesha kwamba alikuwa na uhakika wa jambo hilo, alisoma hadi namba za lori hilo na tela lake kutoka kwenye karatasi aliyokuwa ameshika mkononi, kisha akasema kuwa lori hilo lilikamatwa katika mji mdogo wa Tunduma, mkoa wa Mbeya wakati likiingia nchini kutoka Lusaka, Zambia, Lakini baada ya polisi kuchukua hatua za haraka kulikamata, kisha wakalipekua hadharani huku wananchi wakishuhudia pale pale Tunduma, kilichokutwa ndani ya lori ni shehena ya vipodozi vya kinamama na sabuni za manukato,” alisema Nape.
Nape aliongeza kuwa, siku chache baadaye, Dk. Slaa akatangaza kuwa Rais Kikwete alikesha katika hoteli ya Lakairo, Mwanza akiweka mikakati ya kuiba kura siku ya uchaguzi huo ili ashinde.
Alitoa mfano mwingine kuwa ni mwaka 2011, akisema Dk. Slaa alimzushia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yohana Balele, lakini baadaye iligundulika alikuwa mzima.
MTANZANIA
Tuhuma za mauaji ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, zimeendelea kutikisa pembe za nchi huku mlinzi wake binafsi, Khalid Kagenzi, akitoboa siri za mkasa huo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, kudai mlinzi huyo alikuwa akitumiwa na vyombo vya usalama kwa lengo la kumuua Dk. Slaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kagenzi alisema hausiki na mpango huo ila kuna watu ndani ya Chadema wamekuwa wakimtuhumu bila kutoa uthibitisho wa madai hayo.
Akiwa amefuatana na mtoto wake wa kiume katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, alisema taarifa iliyotolewa Machi 8, mwaka huu kwa waandishi aliiandika yeye kwa kushinikizwa baada ya kupigwa na kuteswa, huku akitishiwa kuuawa na walinzi wenzake wa Chadema.
Alisema Machi 7, mwaka huu aliitwa katika ofisi ya Makao Makuu Chadema ambako aliingizwa katika chumba kilichokuwa na watu watano aliowatambua kwa majina ambao ni Boniface Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo, Hemedi Sambura, Benson Mramba, na watu wengine wawili aliowataja kwa majina moja moja ya Jumanne na Mamba.
Kagenzi alisema baada ya kuingizwa ndani ya chumba hicho, aliona begi lililokuwa limehifadhiwa bisibisi, kisu, bikari na ‘plies’ ambazo walizitumia kumpiga na kumtesa.
“Ndani ya chumba hicho waliniweka kwenye kona na sikuwa na wasiwasi na kuniamuru ‘weka vitu vyako hapo’, nikawajibu hawana sheria ya kuniambia hivyo kama kuna tatizo waniambie.
“Beni alinyanyuka na kunipiga teke la ubavuni, tena teke la nguvu, sijakaa sawa akanipiga teke jingine na kunibamiza na mbao alizokuwa amezifunga mikononi, nikaanguka chini.
MTANZANIA
Wakazi wa Endarasha nchini Kenya wanaishi kwa shaka kubwa kutokana na nyani na tumbili waliopo katika hifadhi ya Taifa iliyo jirani na makazi yao kuwanyanyasa wanawake pekee huku mmoja akivuliwa nguo wakati alipokuwa shambani.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Ester Wangui ameeleza alichoshuhudia juzi baada ya makundi ya nyani na tumbili wanakadiriwa kuwa 50 kutoka katika hifadhi hiyo kuvamia katika mashamba yao kwa wakato mmoja.
Katika tukio hilo mwanamke huyo alishambuliwa na nyani hao wa kiume ambao walikuwa 10 ambao walikuwa wakinguruma kwa sauti kubwa huku wakiwa wameshika sehemu zao za siri huku wakimtisha.
Mwanamke mwingine alishambuliwa na kuvuliwa nguo wakati alipojaribu kuwazuia nyani hao wasivamie shamba lake.
Walisema nyani hao wamekuwa wakiongezeka katika makazi ya watu kutokana na kupata chakula kingi tofauti na wakiwa ndani ya hifadhi hiyo.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook