MWANANCHI
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Mosha Mahona ameuawa na wananchi baada ya kuwachoma kwa kisu abiria watano waliokuwa kwenye daladala linalofanya safari zake kati ya Posta na Ubungo Simu 2000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa moja usiku katika eneo la Magomeni Usalama na Mahona aliuawa kwa kushambuliwa na wananchi baada ya kudhuru abiria wenzake.
Kamanda Wambura alisema Mahona alikuwa ndani ya daladala hilo lililokuwa likitokea Posta kwenda Kituo cha Simu 2000 ndipo alipotoa kisu hicho na kuwashambulia wenzake sehemu mbalimbali ya miili yao.
“Mahona aliuawa na wananchi baada ya kuwachoma kwa visu abiria watano ambao walipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu. Majeruhi hao wanaendelea vizuri,” Wambura.
Wambura alisema baada ya Mahona kufanya kitendo hicho walianza kumshambulia na kusababisha kifo chake.
Aliwataja abiria waliochomwa visu kuwa ni; Daudi Mwenera, Geogre Nomani, Bakari Andrew, Zawadi Mwaipopo na Eda Kiwege.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi ili kujua sababu ya marehemu huyo kufanya kitendo hicho na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Hilo ni tukio la kwanza la aina yake kwa abiria kuchoma visu wenzake.
MWANANCHI
Mbunge wa Viti Maalum alihama juzi CCM na kujiunga Chadema, Ester Bulaya amesema licha ya kuahidiwa vyeo vingi ukiwamo uwaziri na ukuu wa wilaya ili asihame CCM, aliamua kuviacha ili aweze kuwasaidia Watanzania wa chini ambao wameonewa na serikali ya chama hicho kwa miaka 50 iliyopita.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyikia katika Viwanja vya Stendi ya zamani mjini Bunda jana, Bulaya alisema wakati chama chake cha zamani kilipogundua mikakati yake ya kuhamia Chadema, makada wake walimwendea wakimsihi asitoke, bali abakie ili apatiwe ukuu wa wilaya au uwaziri.
Bulaya aliyeambatana na Mbunge wa Kahama, James Lembeli ambaye pia alijiunga na Chadema juzi, alisema baada ya kutafakari kwa muda mrefu uhalisia wa maisha ya Watanzania hasa wa vijijini na jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekuwa ikiwatendea, aliamua kuachana na ahadi hizo na kujiunga na Chadema kwa kuwa inalenga kuwakomboa Watanzania.
“Ngojeni niwaambie, niliahidiwa ukuu wa wilaya na uwaziri ilimradi tu nisihame CCM. Lakini nikaona yote hayo ni upuuzi, bali cha muhimu ni kuwakomboa Watanzania, nikaachana nayo yote nikaja Chadema,” alisema.
Bulaya aliyejigamba kukulia na kufanya kazi ndani ya CCM, alisema chama hicho hakina sera zozote za kuwakomboa Watanzania badala yake kuna za kuwanufaisha wachache, jambo ambali yeye na Lembeli hawakulitaka.
Bulaya alitangaza azma yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini, akisema tayari ameshajaza fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo.
“Niwaambie tu kwamba nimeshajaza fomu na kuirejesha na kesho (leo) nitashiriki kura za maoni. Inshallaah Mungu akinisimamisha nitagombea nafasi hiyo na nina uhakika wa kushinda,” Bulaya.
Lembeli aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutoipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao, badala yake waichague Chadema kwa nafasi zote bila kumsahau Bulaya kwa ubunge kwa kuwa ni mtu mwadilifu.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee akihutubia mkutano huo aliwataka Watanzania wakubali kula fedha wanazogawa na makada wa CCM ili wachaguliwe kwa nafasi mbalimbali za urais, ubunge na udiwani lakini kura zote waipatie Chadema.
MWANANCHI
Uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chadema katika Jimbo la Bariadi umeahirishwa baada ya kubainika kwa matukio yanayoashiria vitendo vya rushwa.
Wakizungumza baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo, wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya walisema hawataki kuingiliwa na virusi vya rushwa ndani ya chama hicho, kwa kuwa hali hiyo italeta mpasuko na makundi.
Wajumbe hao wameutaka uongozi Chadema kuwa makini na wanachama mamluki wanaohama kutoka vyama vingine vya upinzani ili wasikivuruge.
“Hatua ya kuahirishwa kwa uchaguzi inaonyesha ni namna gani chama kilivyo makini ili wanaotoa rushwa wajifunze umakini huu na wananchi waelewe kuwa chama kinatetea wanyonge,” Makula Saguda.
Hata hivyo, mjumbe mwingine, Masanja Lujani alipinga hatua hiyo akisema kuahirishwa uchaguzi ni ubadhilifu ambao haufai akisisitiza kuwa kama wamekamata mtu akiwa anagawa rushwa wangemtoa katika uchaguzi na wengine wakaendelea.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Emmanuel Mbise alisema uchaguzi huo umeahirishwa baada ya kukamata watu wakigawa rushwa kwa baadhi ya wagombea.
“Chadema kinaaminiwa na kinapendwa na watu kwa sababu hakikubaliani na rushwa, kwa mujibu wa katiba na mamlaka niliyopewa, nimeamua kuahirisha uchaguzi hadi utakapotangazwa tena kutokana na uchaguzi huu kutawaliwa na rushwa,” Mbise.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Wilson Mshuda ambaye pia ni mgombea katika jimbo hilo alisema: “Hatuwezi kunyamaza kimya, hata katiba ya chama kuanzia ukurasa wa 86 inaongelea mgombea ambaye ataonekana kutoa rushwa kwa wajumbe kuwa atakuwa amejiondoa katika kinyang’anyiro.”
Jimbo la Bariadi lina wagombea 12 ambao ni Godwin Simba, Mshuda, Masanja Madoshi, Seni Silanga, Manyangu Kulemwa, Zacharia Shigukulu, Maendeleo Makoye, Sweya Makungu, Sitta Mulomo, Wilson Limbu, Slivatus Masanja na Ntemi Ndamo.
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amesema pamoja na kuwa hatagombea nafasi hiyo, CCM isitarajie kulikomboa jimbo hilo.
MWANANCHI
Wakati uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, ukiingia siku ya tatu leo, kasoro lukuki zimeendelea kugubika mchakato huo huku katika baadhi ya vituo wananchi wakizichapa wakigombania kuingia chumba cha kujiandikisha.
Tukio la kutwangana makonde lilitokea katika Kituo cha Shule ya Mwangaza, Gongo la Mboto saa 2.15 asubuhi wakati uandikishaji ulipokuwa ukianza.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema: “Polisi unaowaona wamefika muda si mrefu, wala hawakuwepo hapa tangu asubuhi… ninadhani walipewa taarifa baada ya watu kuanza fujo wakigombania kuingia ndani kujiandikisha,” alisema Magreth John na kuongeza:
“Watu wamepigana kwa sababu wanasema kuna wenzao ambao majina yao hayakuandikwa jana (juzi) halafu wamefika asubuhi wakaanza kuitwa ndani kujiandikisha. Hapo ndipo mzozo ulipoanzisha na ngumi zikafumuka.”
Msimamizi wa kituo hicho, Ramadhani Mshindo alisema mzozo huo ulitokea kwa sababu ya wananchi hao hawakuelewa utaratibu.
“Jana (juzi) jioni wakati tunafunga zoezi hili saa 12.00 jioni kuna watu wengi walikuwa kwenye foleni ambao hawakuandikishwa, kwa hiyo tuliwaandika majina ili leo (jana) wakifika hapa watangulie kuandikishwa kabla ya wengine. Sasa tulivyofika na kuanza kuita majina yao ili waingie kujiandikisha ndipo watu wakaanza fujo na kupigana ikabidi tupige simu polisi ili waje kutuliza ghasia,” alisema Mshindo.
Katika Kituo cha Shule ya Msingi Jica, Tabata wananchi walilalamikia suala la muda kwani waandikishaji walichelewa na hadi saa 4.30 asubuhi, asilimia kubwa ya watu hawakuwa wamepata huduma. “Nimefika hapa saa 12.00 asubuhi lakini hadi sasa sioni dalili ya kuandikishwa leo… Wametuambia wanaanza kuandikisha wale waliobaki jana kwa sababu majina yao yaliandikwa kwa hiyo sisi wa leo tunasubiri kwanza,” alisema Maria Saleh.
Maria alisema uandikishaji unakwenda taratibu kutoka na mashine kugoma mara kwa mara.
Malalamiko kama hayo yalitolewa na wananchi waliokuwa wamefika kujiandikisha katika Kituo cha Shule ya Msingi, Ulongoni, Gongo la Mboto na waandishi wetu walishuhudia watu wengi wakiwa kwenye misururu, wengine wakiwa wamelala pembeni ya kituo hicho baada ya kuchoka kusimama muda mrefu.
Hata hivyo, kwenye kituo hicho, wananchi walijiwekea utaratibu kwamba kila mtu anayefika anaandika namba kwenye daftari na kupewa kikaratasi kidogo chenye namba hiyo ndipo anapanga foleni.
Utaratibu ambao ulisaidia kupunguza usumbufu na kuondoa vuta ni kuvute wakati wa kuingia kwenye chumba cha kujiandikisha.
Lakini licha ya kujiweka utaratibu huo, Ibrahim Kitumbi alisema changamoto ya muda na vifaa ilikuwa palepale.
“Hivi tunavyozungumza watu waliyopewa namba wamefika 2,145. Hawa wameandika majina tu na kupewa namba. Waliojiandikisha tangu jana hawafiki hata 200. Sasa kwa siku nane zilizobaki kweli tunaweza kumaliza kuandikishwa! Huku si kutunyima haki?” alihoji.
Wakati wananchi wakitoa malalamiko hayo, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Ulongoni, Majura Mtalemwa alisema zoezi la uandikishaji linakwenda vizuri tofauti na wananchi wanavyolilalamikia.
Mkazi wa Temeke, Steven Almasi aliyefika kujiandikisha katika Kituo cha Magogoni, Yombo alisema mwaka huu wa uchaguzi kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wananchi kutoshiriki uchaguzi.
Mtendaji wa mtaa huo, Zeddy Zeddy alikiri kuwapo baadhi changamoto kwenye kituo chake ikiwamo uchache wa mashine za kuandikisha.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba alisema wakazi wote wa jiji hili waliojitokeza wataandikishwa hata baada ya siku zilizopangwa kumalizika hivyo hawatakiwi kuwa na hofu.
HABARILEO
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki ameomba mashine za kuandikisha wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki (BVR), ziongezwe katika vituo vyenye matatizo ya mashine hizo na vyenye idadi kubwa ya watu.
Pia, ametaka mafundi wanaoshughulikia ukarabati wa mashine hizo, kuwa karibu na vituo muda wote ili kutatua changamoto hizo.
Amewataka wakazi wa mkoa huo kuwa wavumilivu, kutokana na changamoto kadhaa zilizojitokeza siku ya kwanza ya uandikishaji katika mfumo wa BVR.
Amesisitiza kuwa changamoto hizo, zinaendelea kutatuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema hayo jana baada ya kutembelea vituo katika wilaya zote tatu za Dar es Salaam. Alikiri kukumbana na changamoto kadhaa katika uandikishaji, ikiwa ni pamoja na maeneo mengi mashine za BVR kuelemewa na kushindwa kufanya kazi.
Alisema kwa kawaida mashine hizo, zinatakiwa kuandikisha watu 100 hadi 200, lakini baadhi ya maeneo wanaishia kuandikisha watu 70, kutokana na mashine hizo kuchoka baada ya kufanya kazi mikoani.
Hata hivyo, aliwahakikishia wananchi wote kuwa wataandikishwa na hakuna mtu atakayeachwa. Katika wilaya ya Kinondoni, hali imeendelea vizuri huku changamoto kubwa ikionekana kuwa ni mashine za BVR kusumbua mara kwa mara, jambo linalosababisha kuhudumia watu wachache kwa muda mrefu.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika vituo tofauti vya wilaya hiyo, wananchi walisema hakuna shida yoyote wanayoipata, isipokuwa kulazimika kukaa muda mrefu vituoni, ambapo katika vituo hivyo mpaka kufikia mchana walikuwa wameandikisha kati ya watu 30 hadi 70.
“Foleni ni kubwa kweli lakini watu wengi hawapo, wakifika wanachukua namba na kuondoka, hakuna tatizo lolote isipokuwa hizi mashine mara kwa mara zinagoma na muda unakwenda,” alisema mkazi wa kata ya Ali Maua A, Mohammed Mavula.
Mkazi huyo wa Kijitonyama, akiwa katika kituo cha Serikali ya Mtaa Kijitonyama alisema tangu alipofika katika kituo hicho, hali iko shwari hakukua na tatizo zaidi ya uandikishaji kwenda taratibu, na hivyo kushauri Serikali iongeze na siku za kujiandikisha, akijenga hoja kuwa, Dar es Salaam ina wakazi wengi ikilinganishwa na mikoa mingine nchini.
Hali ya vituo vingi Kinondoni, ilionekana kuwa ni shwari na watu waliokaa kwa utulivu walioridhika kwa utaratibu uliokuwa ukitumika wa aidha kupewa namba na kusubiri huku wengine wakiondoka na kurudi baadaye au kuandikishwa majina yao kwa watu hamsini hamsini au mia moja.
Vituo hivyo havikuwa na watu wengi sana na pia hakukua na misururu ya kutisha kutokana na utaratibu huo kusaidia kupunguza watu kurundikana katika vituo vya kujiandikishia. Hata hivyo kutokana na vituo vingi jana kuandikisha watu wachache kutokana na kusumbua kwa mashine na vifaa kuchelewa kufika vituoni katika baadhi ya vituo, waliokwama juzi ndio walioanza kuhudumiwa.
“Baadhi ya watu wanaamua kuondoka tu kwa sababu wakifika na kukuta namba zimefika mpaka 300 wanakata tamaa na kuondoka zao,” alisema mkazi wa kata ya Kijitonyama Husna Juma.
Ofisa wa Uandikishaji, Farida Kimbanga alisema uandikishaji unakwenda vizuri hata hivyo changamoto za hapa na pale zinaweza kujitokeza, ambazo ni za kawaida na wanazitafutia ufumbuzi mara moja na kwamba hakuna vurugu zozote ambazo zimejitokeza.
Ilala waongezeka Hali kama hiyo ilielezwa kutoka katika Manispaa ya Ilala, ambako hali ilikuwa shwari na idadi ya watu ikizidi kuongezeka. Kwa sehemu kubwa, changamoto ilikuwa katika mashine, kwani uandikishaji ulikuwa wa taratibu. Mathalani, kufikia saa nane baadhi ya vituo viliandikisha watu wasiozidi 50 kuanzia asubuhi.
Katika vituo vilivyoandikisha watu wachache ni vile ambavyo mashine za uandikishaji zilisumbua ikiwemo kutoa picha zinazojirudia. Wakala wa Tume ya Uchaguzi (NEC) katika kituo cha kujiandikisha cha mkoani kilichopo Ilala, Steve Johnson alisema mashine hizo zilifanya kazi asubuhi na baadaye kuanza kutoa picha zinazojirudia hivyo kusitisha uandikishaji kwa mashine moja.
Alisema katika kituo hicho kuna mashine tatu za uandikishaji hivyo kubaki mbili ambazo mpaka mchana ziliandikisha watu 40 huku kwa siku ya jana waliandikisha watu 68 katika kituo hicho.
Nako katika kituo kwa Mtendaji Kata wa Ilala, mpaka mchana walikuwa wameandikisha watu 150 ambao wanakaa mstari kwenye mafungu ya watu kumi kwenye mashine nne zilizopo ukiacha wanawake wajawazito na wenye watoto ambao hawapangi mstari.
Imeelezwa kuwa kwa siku ya jana, hali ilikuwa nzuri kwa uandikishaji kwenda haraka haraka kwani wasimamizi wameishaanza kuzoea kutumia mashine hizo. Katika kituo cha Majani ya Chai, Uwanja wa Ndege alisema hali ni ngumu na mashine zinasumbua kiasi ambacho watu walianza kufanya fujo mpaka askari Polisi walipoingilia kati.
Inaelezwa juzi waliandikisha watu 105, lakini jana, ikiwa ni siku ya pili ya uandikishaji, kufikia mchana waliandikishwa watu 29 tu. Temeke walia na mashine Nako katika Manispaa ya Temeke, watu waliendelea kumiminika vituo vya kuandikisha kupigakura, lakini wengi walijikuta wakikwama katika foleni ndefu, sababu kubwa ikielezwa ni changamoto za mashine pamoja na utaalamu mdogo wa matumizi ya kompyuta.
Mkazi wa Temeke Wailes, Moses Felix alisema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo kuhusiana na uandikishwaji huo unavyoendelea. “Waliokuja kujiandikisha ni wengi, lakini wanaoondoka ambao tayari wamehudumiwa ni wachache hawazidi 30,” alisema Felix.
Mjumbe wa Shina ambaye ni wakala wa CCM katika uandikishwaji huo katika eneo la Miburani, Steven Mkundi alisema changamoto iliyopo ni kukatika kwa ‘network’ kwa mashine hizo.
“Mashine zilizopo mara nyingi network haifanyi kazi inachukua muda mrefu sana huku msururu ukiwa ni mkubwa. Lakini katika eneo hilo wananchi wamejitokeza kwa wingi, wamehamasika,” alisema.
Alisema juzi watu walioandikishwa katika eneo hilo walikuwa ni 95, hadi jana mchana tayari watu 67 walikuwa wameshajiandikisha.
Alisisitiza kuwa tatizo lingine linalojitokeza ni kutokana na uchakavu wa mashine, pamoja na muda wa kuanza kujiandikisha. Imeandikwa na Regina Kumba, Theopista Nsanzugwanko na Lucy Ngowi
HABARILEO
Ziara ya kihistoria ya Rais wa Marekani, Barack Obama nchini Kenya inatarajiwa kusimamisha shughuli nchini kwa muda kupisha ujio wa kiongozi huyo wa taifa kubwa, lenye nguvu za kijeshi, kisiasa na kiuchumi duniani.
Miongoni mwa shughuli zitakazosimama ni usafirishaji wa anga, kwani mamlaka inayosimamia safari za ndege nchini Kenya (KCAA), imetangaza kuwa anga la Kenya leo litafungwa kwa dakika hamsini ili kuruhusu ndege ya Obama kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi.
Kwa mujibu wa shirika hilo, agizo hilo litatekelezwa katika viwanja vyote vya ndege vya Kenya na kuwa anga hiyo itafunguliwa baada ya ndege hiyo ya Rais Obama itakapokuwa imetua.
Shirika hilo limeyaandikia mashirika yote ya ndege na pia kampuni zote za usafiri kuhusiana na agizo hilo na kuwa safari za ndege kadhaa zitacheleweshwa leo na Jumapili, ambapo zitachelewa kwa dakika 40 wakati Rais Obama atakapokuwa akiondoka Kenya kwenda Addis Ababa, Ethiopia.
Awali, Idara ya Polisi nchini Kenya ilikuwa imetangaza kuwa anga lote la Kenya lingefungwa siku tatu kabla ya ziara hiyo. Lakini, kwa mujibu wa KCAA ndege zote zinazopaa chini ya futi 20,000, hazitaruhusiwa kutua katika uwanja wa Jomo Kenyatta na ule wa Wilson mjini Nairobi leo hadi Jumatatu.
Agizo hilo sasa linamaanisha ndege zote ndogo, ambazo huhudumu kati ya Nairobi na Somalia na viwanja vingine vidogo katika kanda ya Afrika Mashariki, hazitaruhusiwa kutua Nairobi hadi mkutano wa kimataifa wa kibiashara ambao Obama atahudhuria utakapomalizika.
Obama anatarajiwa mjini Nairobi siku ya Ijumaa usiku, ambapo anatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo la kibiashara pamoja na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta. `Marufuku’ hiyo inagusa pia baadhi ya barabara muhimu za Jiji la Nairobi, ambazo zitafungwa kupisha ugeni mzito wa Obama ambaye anatua Kenya kwa mara ya kwanza akiwa Rais wa Marekani, licha ya ukweli kwamba ana asili ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Baba wa Rais Obama, Dk Hussein Obama ambaye kwa sasa ni marehemu, ni mwenyeji wa kijiji cha Kogelo ambako rais huyo wa Marekani, amewahi kutembelea kuona ndugu zake kwa upande wa baba.
Licha ya Ubalozi wa Marekani kutangaza kuwa Rais Barack Obama hakusudii kutembelea kijijini Kogelo, Magharibi mwa Kenya, bado matarajio ni makubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo. Kogelo, kijiji ambacho hakikujulikana hata nchini Kenya zaidi ya miaka kumi iliyopita, hivi sasa kinatajwa katika magazeti, redio na televisheni kote duniani, kama nyumbani kwa baba yake Rais Barack Obama, Barack Hussein Obama Senior.
Makaburi ya babu yake Rais Obama, Hussein Onyango Obama na Barack Obama Senior, yamewekwa vigae vipya na tayari kokoto zimemwagwa pembeni kuzuia vumbi iwapo wageni watakuja.
Aidha, makazi ya Mama Sarah Obama, bibi wa Rais Obama yamekuwa yakiboreshwa zaidi, huku wakazi wa kijiji hicho wakihoji sababu za kupuuzwa na serikali ya Marekani, wakidai Obama alistahili kwenda kusalimia ndugu zake.
Hata hivyo, Mama Sarah amedai kuwa alipokutana na Rais Obama Novemba mwaka jana huko Marekani, alimweleza angekuja kuzuru kaburi la baba yake. “Lazima atafika hapa kuona kaburi la baba yake,” alisema Mama Sarah Obama.
HABARILEO
Aliyekuwa mwanachama mashuhuri na mbunge wa miaka mingi kwa tiketi ya CUF, Hamad Rashid ametangaza kukiacha chama hicho na kuhamia chama cha Alliance for Democratic Change (ADC).
Ameahidi kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, endapo chama chake hicho kipya kitamthibitisha.
Aidha, ameelezea kufurahishwa kwa mapokezi aliyoyapata na kuongeza kuwa anashauri vyama vya siasa vya upinzani nchini, vibadilishe mitazamo ili viwe taasisi na kupokezana vijiti kwenye nyadhifa za uongozi.
Rashid aliyasema hayo jana Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa chama hicho wa kupokea wanachama wapya, waliojiunga na ADC, akiwemo yeye, ambaye alipewa kadi namba moja ya chama hicho na kurudisha kadi ya CUF.
Rashid alisema umefika wakati sasa wa vyama vya siasa vya upinzani kubadilisha mtazamo na kuwa taasisi badala ya kuonekana ni chama kinachoongozwa na mtu mmoja, kwani jambo hilo halileti demokrasia wala haki.
“ADC msirudie dhambi ya vyama vingine vya upinzani, tuwe na ukomo wa madaraka na chama kiwe taasisi ambayo uongozi ni kupokezana vijiti, hii ndiyo haki ni moja ya jambo lililonivutia kujiunga na ADC, kuna ukomo wa madaraka, sio zaidi ya miaka 10”, Rashid.
Alisema chama kisichojenga makada wa kurithi ni chama chenye matatizo ya uongozi na kwamba chama ili kiendelee ni lazima kijenge watu watakaorithi baada ya ukomo wa nyadhifa zao kufika na kukitaka ADC, kuhakikisha kinajijenga kuwa taasisi ili kiendelee.
Akizungumzia shutuma zinazotolewa dhidi yake kuwa yeye ni msaliti, alisema hajawahi kuwa msaliti, bali ataendelea kuwa mkweli hata kama ukweli huo unauma. “Nimeitwa msaliti, ila nakumbuka mwaka 1988 nilifukuzwa CCM, nilisema ukweli na hata nilipokuwa CUF, nilisema chama hakiendi kwa sababu kinaongozwa kama mtu binafsi na sio taasisi, na mabilioni ya fedha yaliliwa, sasa huo ndio usaliti?” Rashid.
Aliwataka ADC na wanachama wake, kutomkasirikia mwanachama yeyote atakayeamua kwa ridhaa yake kuhamia chama kingine, kwani ana haki ya kufanya hivyo na kamwe wasiwaone ni maadui.
Akizungumzia mwelekeo wa siasa nchini, Rashid alisema hivi sasa siasa za Tanzania zimebadilika sana na kuwa siasa za fedha na kwamba ni vyema wananchi wakamuogopa Mungu, na kamwe wasikubali kuhadaiwa na fedha , ili kuchagua viongozi.
“Siasa za Tanzania zimebadilika, zimekuwa siasa za fedha, tafadhalini, msikubali kudanganywa na wagombea wanaotoa fedha, huo sio uadilifu, nilijifunza mambo matatu kwa Hayati Mwalimu Nyerere, uadilifu, kusimamia maamuzi na kuwa karibu na watu, hivi ndivyo vitu vya msingi kwa kiongozi na sio fedha”,Rashid.
Awali, Mwenyekiti wa Chama hicho, Said Miraji alisema chama kitasimamisha wagombea katika uchaguzi ujao kwenye nafasi mbalimbali kuanzia ya urais hadi madiwani, na kuwataka wanachama wake hususan wanawake kujitokeza kuwania nyadhifa hizo.
NIPASHE
Watu kumi wamekufa kwenye ajali ya basi la Simiyu lenye namba za usajili T.318 ABM iliyotokea juzi maeneo ya Chalinze wilayani Chamwino mkoani hapa huku majeruhi na mashuhuda wakisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva.
Basi hilo ambalo lilikuwa likitokea Mwanza kuelekea Dar es Salaam ilitokea juzi saa 12:30 jioni.
Baadhi ya majeruhi hao ambao walisema ajali hiyo ilitokana na mwendo kasi wa dereva.
Mmoja wa majeruhi hao, Sawika Saganda (40), alisema watu wengi waliumia na kufa kutokana na kubanwa na viti.
Aidha, alisema wakati gari likiwa kwenye mwendo mkali tairi lilipasuka na ndipo gari lilisererekea msituni na kugonga mbuyu.
Kwa upande wa mashuhuda wa ajali hiyo, walisema ajali hiyo ilitokana na mwendo kasi wa dereva uliyochangia kwa kiasi kikubwa gari kupoteza muelekeo na kuingia porini na kugonga mti.
Lucy Kalulu alisema chanzo kikubwa cha ajali hiyo kilisababishwa na mwendo kasi na ndiyo maana tairi likapasuka na gari kupoteza muelekeo.
Alisema gari lisingekuwa na mwendo kasi lingeyumba kidogo na kutulia bila ya kuingia msituni.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya alithibitisha kupokea maiti nane na majeruhi 55.
Alisema maiti mbili ziliongezeka kutoka kwa majeruhi 55 ambao walikuwa kwenye matibabu.
Alisema waliokufa wakiwa hospitalini hapo ni mwanamke mjamzito, Rukia Mkupe na Mussa Kashinde.
Mbali na hao, wengine ni Elias Mibawa, Mfungo Matutu, Emmanuel Binamungu, Salum Ramadhan, Nestory Ambloz, Shimba Masungu, Maduhu Lushanga na Charles Mahushi.
NIPASHE
Shinikizo dhidi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, la kumtaka akihame Chama Cha Mapinduzi (CCM) linazidi kuongezeka na katika timu yake ya ndani ni watu wawili tu wanaonekana kumtaka abakie ndani ya chama hicho.
Habari za ndani ya vikao vya kujadili hatua za kuchukuliwa na Lowassa baada ya jina lake kukatwa kwenye mchakato wa kugombea urais kupitia CCM, zinasema kuwa wandani wake wanaamini kuwa hana atakachopata kama ataendelea kubaki kwenye chama hicho tawala.
“Kaka sikiliza, inavyoelekea shinikizo dhidi ya Lowassa ni kubwa sana. Watu wake wa ndani wanataka aondoke CCM. Wanaona kama amedhalilishwa mno,” kilisema chanzo chetu ndani ya vikao hivyo.
Chanzo hicho kilichoomba kutokutajwa jina kwa sasa, kilisema kuwa watu wake wa ndani wanaamini Lowassa akiendelea kubaki CCM atakuwa amewavunja moyo wale wote waliompigania, hasa vijana waliojaa matumaini ya kumuona akiongoza taifa hili.
Wandani wa Lowassa wanaamini kuwa kama akiamua kujiunga na chama chenye nguvu cha upinzani anaweza kutimiza ndoto yake ya kuwatumikia Watanzania kama rais wa awamu ya tano.
Chanzo chetu kinasema kuwa Lowassa mwenyewe amekwisha kuamua kufanya uamuzi mgumu, ila kuna msuguano juu ya namna ya kuondoka CCM.
Taarifa zaidi zinasema kuwa watu wawili katika timu ya ndani ya Lowassa ndio wanaelekea kuwa na mawazo tofauti. Hawa ni Rostam Aziz, mwanasiasa na mfanyabiashara mashuhuri nchini na mtu mwingine anayetofautiana na mkakati huu mpya wa kung’oka CCM ni mkewe, Mama Regina Lowassa.
Chanzo chetu kinasema kuwa wawili hao wanaamini mapigo ambayo Lowassa amekumbana nayo ni mengi na yanatosha, kwa maana hiyo ingefaa tu apumzike.
“Sijui ni kwa nini RA (Rostam Aziz) anakuwa skeptical (shaka). Si unakumbuka ndiye aliyesema amechoshwa na siasa uchwara… sasa sijui kwa nini anapunguza makali,” chanzo kilisema.
Hata hivyo, vyanzo vyetu vinaongeza kuwa pamoja na upinzani huo Lowassa anadaiwa kuwa amekwisha kuamua na kinachosubiriwa sasa ni muda tu wa kutamka anakokwenda.
Wakati hali ikiwa hivyo ndani ya kambi ya Lowassa, kuna taarifa za kuaminika kuwa kumekuwa na mashauriano baina ya watu wake na viongozi waandamizi wa kambi ya upinzani juu ya mwelekeo wake wa kisiasa.
Mwandani mwingine katika kambi ya Lowassa alisema kimsingi yeye (Lowassa) amekwisha kuamua, anachofanya ni kuona kwamba watu wake wa karibu hawadhuriki na uamuzi wake huo.
Takriban wiki mbili sasa, Lowassa amekuwa na jambo kubwa moyoni analitaka kuwaambia Watanzania.
Nitakutumia stori zote ukibonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie