MTANZANIA
Wabunge wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametajwa kukataa uteuzi wa nafasi ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne zilizokuwa wazi, imebainika.
Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12, mwaka huu.
Wabunge hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini walidai kuwa kasi ya Rais Magufuli inawatia hofu.
“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito na kwangu ni ngumu na nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya taarifa hizi nasikia na wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.
“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada ya kupima nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge wangu,” alisema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri, Desemba 10, mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo na kwamba anaendelea kuwatafuta.
Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliteua manaibu waziri wa wizara hizo, huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake baadaye atakapomaliza mchakato.
Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo naibu wake ni Dk. Ashatu Kijaji.
Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii, ambayo naibu wake ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.
MTANZANIA
Mkazi wa Ilala Mtaa wa Lindi, Hafidhi Ally, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni akikabiliwa na tuhuma za kuvamia kisha kuingia nyumbani kwa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.
Mbele ya Hakimu Ester Kihiyo, karani wa mahakama hiyo, Mosses Mchome, alidai kwamba mtuhumiwa alifanya kosa hilo Desemba 10, mwaka huu saa 7:30 usiku nyumbani kwa Mzee Mwinyi, Mikocheni B, Dar es Salaam.
Karani Mchome aliiambia mahakama hiyo kwamba, Hafidhi aliingia hadi ndani ya nyumba hiyo bila ruksa kutoka kwa mlinzi aliyekuwapo kwenye lindo, Nuru Saidi, ambapo alimweleza kwamba hana mahali pa kuishi.
“Mtuhumiwa ulikaidi amri ya mlinzi aliyekuwepo zamu siku hiyo, aliyekutaka urudi ulipotoka, kisha ulisisitiza kwamba huna sehemu ya kuishi, lakini pia wewe ni mtoto wa rais huyo mstaafu wakati huo ukielekea ndani kitu ambacho ni kinyume cha sheria,” alidai Mchome.
Mtuhumiwa alikana kosa hilo na upelelezi bado unaendelea.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 28, mwaka huu na mtuhumiwa alirejeshwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo alitakiwa apeleke wadhamini wawili waaminifu wenye barua kutoka kwa ofisa mtendaji wa kata anakoishi.
MTANZANIA
Mtu mmoja amefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa, akiwamo askari polisi mmoja baada ya kutokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Dihinda, Kata ya Kanga, Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Dihinda, Hariri Kilama, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 11, saa 11 jioni.
Kwa mujibu wa Kilama, tukio hilo lilisababishwa na mfugaji mmoja aliyejulikana kwa jina la Shaban Ramadhan, kuingiza ng’ombe wake katika shamba la mkulima aliyetambuliwa kwa jina la Bakari Mlunguza ambao waliharibu mazao.
“Baada ya uharibifu wa mazao hayo, uongozi wa kijiji ulimwita Bwana Shamba wa Kijiji, Mathew Limbanywa, kwa ajili ya kufanya tathimini ya mazao yaliyoharibiwa na mifugo hiyo.
“Baada ya tathmini hiyo, ilibainika, kuwa uharibifu uliofanyika ulikuwa mdogo na bwana shamba huyo aliomba suluhu ifanyike ili kutatua mgogoro huo.
“Pande hizo zilipokaa pamoja, mkulima aliomba alipwe fidia ya shilingi laki tatu, lakini mfugaji alikataa na kusema yupo tayari kulipa shilingi laki mbili.
“Makubaliano hayo yalipofanyika saa nane katika ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Wiliam Masanyika, mfugaji aliondoka na saa 11 jioni alirudi na kundi la wenzake na kuanza kupiga miruzi ya kuita ng’ombe wake waliokuwa chini ya ulinzi ofisini hapo.
“Wakulima walipoona kuna dalili za mapigano, nao walijibu mapigo, ambapo wafugaji walimpiga mkulima mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Mohamed ambaye alifariki dunia wakati akipelekwa katika Hospitali ya Mission ya Bwagala wilayani humo.
“Pamoja na mauaji hayo, ng’ombe 71 nao waliuawa na wengine 120 walijeruhiwa vibaya na wakulima hao,” alisema Kilama.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, Mwigulu Nchemba, aliliagiza Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kuimarisha ulinzi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuwakamata waliohusika katika vurugu hizo.
Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, alisema polisi mkoani hapa wanawashikilia watu 19 wakiwamo watatu wanaodaiwa kuwaua ng’ombe hao kwa kuwakatakata kwa mapanga
MWANANCHI
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema watu wanaomiliki mashamba bila kuyaendeleza huku wakiyatumia kama dhamana ya kukopea fedha benki watanyang’anywa.
Lukuvi, akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuripoti kazini jana pamoja na naibu wake, Angelina Mabula, alisema kuna watu wamehodhi mashamba makubwa lakini hawayaendelezi, hawayalipii kodi, na mbaya zaidi wanayatumia kukopa fedha benki.
“Mkuu wa idara anayehusika na ardhi ninaomba Jumatatu ijayo orodha ya watu tuliowapa ardhi lakini wameitumia kuombea mikopo ambayo wanaitumia kwa shughuli nyingine.
Hao nitalala nao mbele,” alisema Lukuvi baada ya kujitambulisha kwa wakuu wa idara za wizara hiyo.
“Nipeni pia orodha ya watu wanaotakiwa kulipa kodi ya ardhi lakini hawalipi na tukikutana wiki ijayo nielezeni taratibu zinazotakiwa kuchukuliwa dhidi yao,” alisisitiza.
Akisisitiza kuhusu hilo, Lukuvi alisema wiki ijayo atakwenda kuchukua shamba lililohodhiwa na mwekezaji lenye ekari 1,600 huko Mbarali mkoani Mbeya na kuwarudishia wananchi.
Japokuwa Lukuvi hakumtaja mwekezaji atakayenyang’anywa shamba hilo wilayani Mbarali, lakini shamba la ukubwa huo lililokuwa na mgogoro kwa muda mrefu ni la Kapunga.
Akiwa kwenye kampeni mkoani Mbeya, mgombea urais wa CCM ambaye sasa ni Rais John Magufuli, aliahidi kurejesha shamba hilo kwa wananchi ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu.
Aidha, Lukuvi aliwaagiza maofisa hao kuwasiliana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuangalia wawekezaji waliopewa ardhi kama wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Tukikutana Jumatatu ijayo nipewe taarifa za kila mwekezaji na ukubwa wa ardhi aliyopewa; aliomba kwa madhumuni gani, na je, anaitumia ardhi hiyo kwa madhumuni aliyoombea?” alihoji. Kuhusu upimaji wa ardhi,
Lukuvi alisema asilimia 10 ya ardhi nchini ndiyo imepimwa na kwamba juhudi zinahitajika ili kupima ardhi zaidi. Tunataka tukikutana wiki ijayo, ofisa anayehusika na upimaji aje na mpango wa upimaji ardhi na umilikishaji na atueleze utagharimu kiasi gani ili tuweze kuona serikali itawekeza vipi katika upimaji wa ardhi nchi nzima,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa nyumba za kupangisha, Lukuvi alisema kumeibuka kampuni nyingi zinazofanya biashara ya kujenga nyumba kubwa na kuzipangisha lakini hakuna chombo chochote cha serikali kinachosimamia sekta hiyo. “Hii ni biashara kubwa ambayo inakua siku hadi siku, hivyo ni lazima sasa wizara isimamie kwa kuweka chombo maalumu. Hivi sasa biashara inafanyika lakini hatupati kodi kwa sababu si rasmi,” alisema.
Waziri Lukuvi alimtaka mkurugenzi wa nyumba wa wizara hiyo kuandaa mpango wa namna ya kuwasaidia watu maskini ili kuwa na nyumba bora.
“Tunataka atueleze serikali ifanye nini ili kuwasaidia wananchi maskini kuwa na nyumba bora ili waondokane na nyumba zilizoezekwa kwa nyasi,” alisema.
MWANANCHI
Wizara ya Nishati na Madini, imezindua matumizi ya mfumo mpya wa malipo ya ada za leseni za madini kwa njia ya kielektroniki (OMCTP) Kaimu Kamishna Mkuu wa Madini, John Nayopa jana alisema mfumo huo ulianza kutumika wiki iliyopita na utawawezesha wateja kutuma maombi ya leseni na taarifa za utendaji kazi kwa njia ya mtandao.
“Mfumo huu ni salama kwa fedha za wateja na kuanzia sasa malipo ya ada za leseni yatafanyika kwa njia ya mtandao pekee. Ofisi zetu za madini zitatoa msaada kwa wateja wanaohitaji maelekezo,” alisema.
Alisema utawawezesha pia wateja kupata ramani za kijiolojia, takwimu mbalimbali za madini na kufanya malipo kwa njia ya miamala ya simu za mkononi, Maxmalipo na kupitia benki (EFT).
Nayopa amewataka wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya madini na kuchakata mchanga wenye madini ili wanufaike na Serikali iongeze mapato kwa kupitia ulipaji wa kodi.
Mfumo huo unalenga kurahisisha utoaji wa leseni wachimbaji wadogo, kupunguza mlundikano wa maombi ofisi za madini, kurahisisha mawasiliano kati ya wizara na wamiliki, kujua taarifa za leseni na utoaji wa taarifa za madini kwa wakati
MWANANCHI
Mradi wa kuchakata gesi asilia kutoka Madimba MtwaraSongosongo hadi Dar es Salaam umekamilika na kuwezesha uzalishaji umeme katika mitambo ya Kinyerezi, Ubungo, Tegeta na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Kwa sasa mradi huo unazalisha asilimia 70 ya umeme wote unaotumika nchini kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC), Dk James Matagio alisema jana kuwa nchi inaelekea katika uchumi wa gesi kutoka katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta na maji. Alisema ujenzi wa bomba jipya la gesi umeongeza uzalishaji kwa asilimia 30.
Dk Matagio lisema mradi wa usambazaji gesi asilia katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam pia unalenga kusambaza gesi katika nyumba 30,000 na magari 8,000.
Alisema upembuzi yakinifu na usanifu wa michoro umekamilika na kwa sasa wanatafuta fedha kutekeleza mradi unaotarajia kugharimu Dola 150 za Marekani.
Meneja wa Mawasiliano wa TPDC, Maria Msellemu alisema kutokana na ugunduzi wa mafuta nchini Uganda, Serikali ya nchi hiyo ilitia saini makubaliano na Tanzania kwa kushirikiana na TPDC na Kampuni ya Total.
Alisema makubaliano hayo yanalenga kuangalia uwezekano wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka nchini humo kupitia Bandari ya Tanga hadi kwenye soko la nje.
“Tumeanzisha kampuni tanzu za Gaso ambayo inashughulikia gesi, Copec uagizaji wa mafuta na Kampuni ya International Business biashara za kimataifa,” alisema Msellemu.
MWANANCHI
Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), kimekamata shehena ya makonyo na karafuu kavu iliyodaiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa njia ya magendo katika Bandari ya Milango Mikavu kisiwani hapa.
Kamanda wa KMKM Pemba, Silima Haji Haji alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku. Alisema watu waliokuwa wakivusha shehena hiyo walikimbia na kutelekeza magunia 31 za makonyo na manne ya karafuu kavu baada ya kuwaona askari wa kikosi hicho wakienda kuwakamata.
Alisema kabla ya tukio hilo, askari waliokuwa doria waliwatilia wasiwasi na walipowafuatilia watuhumiwa hao walikimbia.
Kamanda Silima alisema katika kipindi hiki ambacho karafuu zinaendelea kuchumwa, askari wake wameongeza ulinzi baharini na nchi kavu ili kuwadhibiti watu wanaotaka kuhujumu uchumi wa nchi kwa masilahi yao binafsi.
Mdhamini wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) Pemba, Abdalla Ali Ussi amepongeza juhudi zinazochukuliwa na kikosi cha KMKM kupambana na biashara ya magendo ya karafuu.
Aliwataka wananchi kujiepusha na biashara hiyo haramu inayowanufaisha kwa kuwa inadhoofisha uchumi wa nchi. Alisema wananchi wameitikia wito wa Serikali wa kuuza karafuu katika vituo vya ZSTC na kwamba fedha zinazopatikana hutumika katika kukuza maendeleo.
Baadhi ya wananchi wanaouza karafuu katika Kituo cha Shirika Bandarini Wete, wameviomba vyombo husika kufanya uchunguzi ili watuhumiwa wakamatwe.
Mmoja wa wakazi hao, Yussuf Said Rashid alisema ni vema Serikali kupitia ZSTC kuandaa utaratibu maalumu wa kuwakagua wananchi wenye mikarafuu ili kujiridhisha kama wanaziuza kwenye vituo vya shirika hilo.
Alisema vitendo vya magendo vinatakiwa kukomeshwa kwa kuweka mikakati kabambe ya kuvidhibiti ikiwamo wananchi kutoa taarifa wanapoona matukio kama hayo.
MWANANCHI
Maandalizi ya upangaji wa ada elekezi kwa shule binafsi nchini yameibua mvutano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (Tamongsco) baada ya kulalamikia kutopewa nafasi ya ushiriki katika hatua za awali.
Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamini Nkonya alisema jana kuwa chama hicho kiliwachagua mawakili wake wanne kwa ajili ya kutoa ushirikiano kwa wizara hiyo katika upangaji na uchambuzi wa ada elekezi, lakini haijawatumia.
Alisema Serikali imekuwa ikiwatumia wamiliki wa shule binafsi wasiokuwa na uwakilishi wa mawazo ya chama hicho. Waliochaguliwa na chama hicho kuwakilisha maoni yao ni mwenyekiti wake, Mrinde Mnzava, makamu mwenyekiti Jeremiah Bwegenyeza, Katibu mkuu, Benjamin Nkonya na mhasibu, Mapenzi Yona.
Hata hivyo, Kamishina wa Elimu Wizara hiyo, Profesa Eusella Bhalalusesa alipinga ofisi yake kupokea majina ya wawakilishi wa chama hicho.
Alisema utafiti bado unaendelea, hivyo wanayo nafasi ya kuwasilisha maoni yao. “Sijapata majina yao, lakini kwa nini tugombanie fito wakati nyumba ni moja? Wadau ni wengi na siyo rahisi kumfikia kila mmoja, wataalamu watakapokamilisha ripoti yao kabla ya mwaka wa masomo 2016, tutaichambua na wadau wote kabla ya kuanza majaribio yake.
“Lakini katibu huyo wa Tamongsco (Benjamini Nkonya) nilimuona kwenye televisheni akisema wameshiriki vizuri kutoa maoni yao,” alidai Profesa Bhalalusesa.
Profesa Bhalalusesa alitaja baadhi ya vigezo vitakavyotumika kupanga ada elekezi kuwa ni huduma zinazotolewa na shule, eneo la shule inakopatikana na mmiliki wa shule husika.
Alipoulizwa kuhusu kutenganisha mtoa huduma na mfanyabiashara ili kutoza kodi alisema: “Ndiko tunaelekea huko, tutaangalia shule inayotoa huduma na inayofanya biashara ili iweze kutozwa kodi.”
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.