Mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) ameibuka kidedea na kwa kupata kura 54,609 na kumgaragaza mgombea wa Chadema Emmanuel Ole Landey aliyepata kura 8,782.
Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Simanjiro, Yefred Myenzi akitangaza matokeo hayo mji mdogo wa Orkesumet amesema wapiga kura waliojiandikisha ni 133,086.
Myenzi amesema kati ya hao waliojiandikisha, waliopiga kura ni 64,238 na kura halali ni 63,391 na kura zilizokataliwa ni 847.
Amesema kwa upande wa wagombea udiwani, CCM imepata kata zote 18 kwani awali wagombea nane walipita bila kupingwa hivyo ikashinda kwenye kata 10 kulikokuwa na wagombea wa CHADEMA.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa hati ya ushindi wa nafasi hiyo, mbunge mteule wa jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka aliwashukuru wananchi wote kwa kumpatia fursa hiyo ya kuwa mwakilishi wao Bungeni.
“Imani huzaa imani, ninawaahidi kuwapa utumishi uliotukuka sawa sawa na dhamira yenu ya dhati mliyonipa kwa kunichagua kwa kura nyingi takribani asilimia tisini hivyo baada ya kuapishwa nitaanza kuwatumikia kikamilifu japokuwa nimeanza kabla ya kuapishwa” Ole Sendeka.
Amewashukuru wananchi wa jimbo la Simanjiro kwa kumpatia kura nyingi za kishindo mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho Dkt. John Pombe Magufuli kwani wametekeleza ahadi yao kuwa watampa kura nyingi za ndiyo.
“Mgombea urais wa CCM Dk Magufuli ameongoza kwenye vituo vyote katika kata zote 18 za Jimbo la Simanjiro kuanzia Mirerani, Naisinyai, Orkesumet, Naberera , Ojloro Namba tano, Edonyongijape, Ngorika, Msitu wa Tembo, kila mahali” Ole Sendeka