JAMBO LEO
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe amewataka wakazi wa Kigoma kutosikitishwa na mambo yanayomkabili kwa sasa ila wamuunge mkono kwa hatua yoyote atakayoichukua kwa kuwa ni wanasisasa wengi wamepitia katika misukosuko kama yake.
Zitto ametoa kauli hiyo Kigoma alipokutana na viongozi 250 wa vijiji Kigoma alipokutana nao jana.
“Msinililie mimi kwa kuwa haya ni mapito ya kila mwanasiasa makini, wengi walitofautiana na vyama vyao kwa sababu ya ya maslahi ya mataifa yao.. hivyo jukumu kubwa ni kuniunga mkono…”– Zitto Kabwe.
Mbunge huyo amesema hadi sana hajapewa taarifa yoyote ya kusitishwa kwa Ubunge wake, lolote likitokea atarudi kuwafahamisha juu ya uamuzi wake.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza kuchunguza malalamiko ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa ya kutaka kulishwa sumu na Mlinzi wake.
Madai hayo ambayo yamekuwa gumzo katika vyombo vya habari wiki hii huku wananchi wakihoji uhalisia wake, yamemuhusisha mlinzi huyo wa Dk Slaa huku yeye mwenyewe akikataa tuhuma hizo na kudai kuwa ameteswa na walinzi wa CHADEMA.
Mlinzi wa Dk. Slaa alidai kuwa ana majeraha mwilini yaliyotokana na mateso aliyofanyiwa akiwa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama wa CHADEMA.
Kamanda Kova amesema kuna mambo mawili yanafanyiwa uchunguzi likiwemo la mlinzi Khalid Kagenzi na la pili ni dhidi ya watuhumiwa wanaodaiwa kumtesa kwa kumshambulia mlinzi huyo na kumsababishia majeraha mwilini mwake ambao ni Boniface Jacob ambae ni diwani kata ya Ubungo, Hemed Ally Sabula ambae ni Afisa Usalama wa CHADEMA na Benson Mramba mkazi wa Tabata Kisukuru ambaye ni Afisa Utawala wa CHADEMA.
Kova amesema shauri la kesi hiyo litafikishwa mahakamani kupitia kwa wakili wa serikali ili kujiridhisha kisheria na kutoa maamuzi kuhusu mashtaka yao.
TANZANIA DAIMA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imenusa harufu ya ufisadi kwenye kivuko cha Mv Dar es Salaam ambacho kinatarajiwa kuanza safari kutoka Dar kwenda Bagamoyo kupitia Kawe na Mbezi Beach ambapo Kamati hiyo imebaini kuwa kivuko hicho ni chakavu na cha zamani.
Kamati hiyo imebaini hayo wakati wa ziara ya kukikagua ambayo ilifanywa wakiwa wameongozana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Greyson Lwenje huku Mbunge Haroub Shamsi akisema kwamba thamani ya pesa zilizotajwa na uhalisia wake ni tofauti hivyo waliohusika kwenye manunuzi hayo wachunguzwe.
“Waheshimiwa Wabunge siwezi kutoa maelezo ya kina hapa maana kuna waandishi wa Habari, tusubiri kufanya kikao chetu wenyewe, nitaeleza kila kitu lakini si hapa…” alijibu Naibu Waziri Lwenje na kufanya Wabunge hao kukasirishwa na kususia kumsikiliza Waziri huyo.
TANZANIA DAIMA
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda, Katavi wamekutwa wakiwa wamepoteza fahamu kwenye bweni lao la na miili yao ikiwa imechanjwa chale bila wao kujitambua.
Mkuu wa Shule hiyo Paza Mwamlima amethibitisha kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia jana shuleni hapo ambapo bweni hilo lilikuwa na jumla ya wanafunzi 40 waliokuwa wamelala.
Siku ya jana asubuhi mwanafunzi mmoja aliwahi kuamka ili awahi namba shuleni akawaacha wenzake wamelala, Walimu walipoona wanafunzi wa bweni hilo hawaonekani walienda na kukuta mlango umefungwa, baada ya kuufungua kwa nguvu walikuta wanafunzi hao wakiwa katika hali hiyo.
MWANANCHI
Hali ya amani katikati ya Jiji la Mwanza jana ilichafuka kutokana Polisi kupambana na wananchi, waliokuwa wakipinga hatua ya madhehebu ya Kihindi ya Swaminarayan kujenga nguzo makutano ya Mtaa wa Lumumba na Makoroboi ili kuzuia watu kukatisha eneo hilo.
Eneo hilo lilikuwa lilikuwa likitumiwa na wamachinga, lakini viongozi wa hekalu hilo walimuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwaondoa kwa sababu walikuwa wakiwabughudhi wakati wa ibada zao ambapo Wamachinga 169 waliondolewa na kupewa eneo la Tanganyika ambako wanaendesha biashara zao na sehemu hiyo kutumiwa na wapiti njia.
Jana wananchi walivamia eneo hilo na kuanza kung’oa nguzo hizo, hali iliyosababisha kuitwa polisi ambao walianza kutupa mabomu ya machozi.
Vurugu hizo zilidumu hadi saa 5:30 asubuhi na kusababisha maeneo ya Msikiti wa Ijumaa, Kituo cha Daladala, Mtaa wa Lumumba na Barabara ya Nyerere yakitawaliwa na moshi wa mabomu ya machozi.
Mtu mmoja amesema eneo hilo ni njia ya umma ambayo inatumiwa na wananchi wengi, hivyo kitendo cha kuweka geti kingezuia matumizi ya njia hiyo ya muda mrefu.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema wanawashikilia vijana 12 waliokuwa wanafanya fujo.
“Tulichofanya tumedhibiti wafanya fujo na sasa tunachunguza iwapo ujenzi huo ulikuwa na kibali,” alisema Kamanda Mlowola.
MWANANCHI
Wanafunzi watano wa Chuo Kikuu UDSM ni miongoni mwa watu walifariki katika ajali ya basi la Majinjah iliyotokea Mafinga siku ya Jumatano baada ya kugongana na lori, huku mwanafunzi mmoja akinusurika na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa Mbeya ambako anapatiwa matibabu mpaka sasa.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Rwekaza Mukandala aliwataja wanafunzi hao waliofariki ambao ni Eric Killeo (mwaka wa tatu), Daud Sosten (mwaka wa tatu), Jeremia Watson (mwaka wa pili), Frank Mbaule (mwaka wa pili) na Didimo Chiwango (mwaka wa pili).
“Uongozi wa Chuo unatoa pole kwa wanafamilia wote pamoja na Jumuiya ya Chuo Kikuu. Tunamtakia mwanafunzi mwingine Rafael Nobert apate nafuu baada ya kujeruhiwa katika ajali hiyo”—Prof. Mukandala.
Wakati huo huo watu kutoka Malawi wamefika nchini kwa lengo la kutambua miili ya ndugu zao kama nao ni miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo huku mpaka sasa kukiwa kumebaki miili ya watu wawili kutambuliwa kati ya watu 50 waliofariki.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook