Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Urusi ulioongozwa na Mjumbe Maalum wa Rais wa Urusi katika masuala ya Afrika ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mikhail Bogdanov, Ikulu Jijini DSM.
Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi hiyo na amemhakikishia kuwa Serikali anayoiongoza inatambua umuhimu wa uhusiano huo na kwamba itauendeleza na kuukuza zaidi hususani katika masuala ya biashara, uwekezaji, utalii na utoaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na miundombinu.
“Naomba ufikishe ujumbe wangu kwa Rais Putin kuwa Watanzania wanaipenda Urusi na tunamkaribisha kuja kutembelea nchi yetu pamoja na wananchi wengine wa Urusi, tunawakaribisha pia wawekezaji waje wawekeza katika fursa mbalimbali zilizopo hapa Tanzania kwa manufaa yetu sote” Rais Magufuli
Kwa upande wake Bogdanov ambaye amewahi kutembelea Tanzania miaka 8 iliyopita ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kasi nzuri ya maendeleo iliyoyapata katika kipindi kifupi na amebainisha kuwa Urusi imedhamiria kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.
Bogdanov amesema Urusi inao mpango mahususi wa kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika kuongeza kasi ya maendeleo na kwamba hivi karibu Tanzania na Urusi zitatiliana saini makubaliano ya kuanzisha tume ya pamoja ya ushirikiano (Joint Permanent Commission – JPC) katika biashara, uwekezaji na uchumi ili rasilimali na fursa zilizopo katika pande zote zitumike kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Prof. Palamagamba Kabudi amesema mazungumzo hayo yamekwenda vizuri na kwamba Tanzania inatarajia tume ya pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Urusi itasaidia kukuza uchumi kupitia madini, gesi na utalii hasa wakati huu ambapo Urusi imeitangaza Tanzania kuwa nchi yenye vivutio bora vya utalii duniani.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi Tanzania nchi Urusi Mej Jen. Mstaafu Simon Mumwi na Balozi wa Urusi nchini Tanzania Yuri Popov.
UWANJA WA DODOMA UTAKUWA KAMA MLIMA KILIMANJARO, UTABEBA WATU ZAIDI LAKI MOJA