Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Msumbuji Filipe Jasinto Nyusi ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala mbalimbali yahusuyo uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji na masuala ya kikanda.
Rais Magufuli amempongeza na kumtakia heri Rais Nyusi na wananchi wote wa Msumbiji kwa Taifa hilo kuadhimisha miaka 45 ya tangu kupata uhuru wake.
Rais Magufuli amemueleza Rais Nyusi kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri wa kidugu, kirafiki na ujirani mwema na Msumbiji kama ulivyoasisiwa na Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Mosës Machel wa Msumbiji katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, viongozi hao wamezungumzia maandalizi ya kupokezana kijiti cha uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa SADC atamkabidhi uenyekiti wa SADC Mhe. Rais Nyusi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa SADC kwa sasa.
Viongozi hao pia wamezungumzia ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) ambapo wamebadilishana mawazo juu ya namna bora ya kukabiliana na ugonjwa huo, hasa namna Tanzania ilivyofanikiwa kupunguza maambukizi yake.