Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani ameitaka Kampuni ya Mbolea ya Yara Tanzania itafute uwezekano wa kupata vipimo vya rutuba ya udongo (Soil Test Kits) na kuviweka katika ngazi ya Kata ili viwasaidie wakulima kujua hali ya udongo kabla hawajalima chochote.
Alisema hatua hiyo itawawezesha wakulima kupima rutuba ya udongo na kupata ushauri wa aina na kiasi cha mbolea wanachopaswa kununua kulingana upungufu na aina za virutubisho vilivyokosekana kwenye udongo.
Balozi Dkt. Batilda ametoa kauli hiyo leo mjini Tabora wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki unaojulikana kwa jina la Yara Connect App.
Alisema uchumi wa Mkoa wa Tabora unategemea kilimo cha mazao ya tumbaku , pamba, mahindi, mpunga, mtama na uwele, karanga na alizeti, mihogo na Viazi vitamu na mazao ya bustani.
Balozi Dkt. Batilda Buriani alisema ili kuzalisha kwa kwa tija katika mazao hayo ni lazima wakulima watumie mbolea za aina mbalimbali na kwa viwango tofauti kulingana na aina ya zao linalolimwa na udongo wa eneo husika.
Alisema Yara Connect itakuwa na manufaa kwa wakulima katika ambapo wataweza kutapa taarifa mbalimbali za kuboresha kilimo kupitia simu janja za mkononi.
Meneja Masuluhisho ya Kijiditaji wa Kampuni ya Yara Tanzania Deodath Mtei alisema lengo la uanzishaji wa mfumo huo ni kuwaunganishaji wasambazaji , wauzaji wa mbolea na wakulima kwa ajili ya kuinua kiwango cha kilimo ili kuzalisha kwa tija mazao mbalimbali.