Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART) Robert Kisena (46) anatarajiwa kuunganishwa na mke wake Frolencia Membe katika kesi ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Bil.2.14.
Mke wa Kisena alifikishwa mahakamani hapo wiki iliyopita, akikabiliwa na mashtaka saba ikiwamo uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha zaidi ya Bilioni 2.4.
Kuunganishwa kwa Kisena na mkewe kumeelezwa na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Wakili Wankyo ameeleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa lakini washitakiwa wawili ambao ni Kulwa Kisena na Charles Seleman hawajafika wanaumwa/
Pia ameeleza kuwa upelelezi shauri hilo haujakamilika, kwa sababu baadhi ya washitakiwa wanatafutwa na mmoja ambaye ni Mke wa Kisena amepatikana na watamuunganisha na mumeo.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 23, 2019 kwa ajili ya kuwaunganisha na mkewe.
Kisena na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka 19 likiwemo la utakatishaji fedha na kuusababishia Mradi wa UDART hasara ya zaidi ya Sh.Bil 2.41
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Kisena(33), Charles Newe(47) na raia wa China, Cheni Shi (32).
Katika mashtaka hayo yakiwemo ya kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa pamoja na shtaka la wizi wakiwa Wakurugenzi.
Pia wanakabiliwa na mashtaka manne ya utakatishaji fedha, kughushi manne, kutoa nyaraka za uongo manne, mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la kuisababishia mradi huo hasara.