Mtoto mweye umri wa miezi miwili ameibiwa baada ya mama yake kudaiwa kunyweshwa dawa za asili na mganga wa kienyeji katika kijiji cha Katororo Wilayani Geita.
Kamanda wa Polisi Mkoani Geita Joseph Konyo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwaonya wazazi kujihami na waganga wa kienyeji wenye dhamira ya kuwafanyia ulaghai.
Kamanda Konyo alimtaja mama aliyeibiwa mtoto kuwa ni Cecilia Timaminye na mtoto aliyeibwa ni Jackson Shija na kudai upelelezi unaendelea huku waganga wawili wakisakwa baada ya kutoroka kufuatia tukio hilo.
Mama wa Mtoto huyo alisema alishawishiwa na wenzake kumpeleka mwanaye kutibiwa ugonjwa wa Bawapopo kwa mganga huyo lakini walipofika huko alipewa dawa ya kuoga na kunywa na kusababisha kupoteza kumbukumbu na kuhisi kuchanganyikiwa.
NIPASHE
Waziri mkuu mstaafu Fredrik Sumaye ametaja sababu tatu za kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao akieleza mojawapo ni kukuza uchumi unaogusa maisha ya Watanzania wote.
Alisema suala la pili ni linalomsukuma kuwania nafasi hiyo ni vita dhidi ya rushwa,ufisadi pamoja na dawa za kulevya na tatu ni kuunda Serikali inayowajibika kwa umma badala ya maslahi binafsi.
“Mimi nimeshasema muda ukiwadia nitajitosa tu kwa maana Watanzania wengi wananiambia nijitose na sina sababu ya kuwakatilia,muda ukifika nitatangaza…kwamba sasa nipo rasmi kwenye kinyang’anyiri hicho,”alisema Sumaye.
Sumaye ambaye anashikilia rekodi ya kukalia kiti cha Uwaziri mkuu kwa miaka 10 mfululizo zaidi ya wengine wote walioshikilia nafasi hiyo chini ya uongozi wa awamu ya tatu ya Mkapa, alisema iwapo atateuliwa kushika wadhifa huo na CCM atakua na vipaumbele vichache ili aweze kusimamia kwa uaminifu.
MWANANCHI
Siku tano baada ya Serikali kukanusha vikali ripoti ya kimataifa ya mazingira iliyoihusisha China na utoroshaji wa meno ya Tembo nchini wakati wa ziara ya Rais wa nchi hiyo Xi Jinping mwaka jana,Shirika la Polisi la kimataifa Interpol tawi la Tanzania limesema linawatafuta raia zaidi ya30 wa China ambao wanatuhumiwa kusafirisha meno ya tembo na kufanya uharamia wa kimazingira katika hifadhi za wanyama.
Kauli ya Interpol inakuja wakati kukiwa na mkanganyiko kuhusu kashfa hiyo iliyosambaa nchi nzima kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa ambavyo hata hivyo Serikali kupitia Ikulu ilikanusha taarifa hiyo.
Kamishna wa Interpol Gustav Babile alisema raia hao wachina wanatafutwa popote pale walipo duniani na watakapokamatwa watafikishwa katika vyombo vya dola.
Alisema majina ya idadi kamili ya Wachina wanaotafutwa ipo na endapo kuna umuhimu wa kutajwa,yatangazwa kwani tayari wameweka majina ya raia wawili wa nchini humo ambao wanasakwa kwa kusafirisha meno ya tembo.
MWANANCHI
Wafuasi wa Chadema Wilayani Mpanda jana walilazimika kutafuta vichochoro vya kukimbilia baada ya polisi kusambaratisha kwa mabomu ya machozi maandamano ya kumsindikiza Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe baada ya mkutano.
Patashika hiyo ilitokea baada ya mkutano kumalizika na wafuasi wake kutaka kumsindikiza hotelini jambo ambalo askari hawakukubaliana nalo.
Baada ya wananchi hao kuanza maandamano,Polisi walifyatua mabomu takribani15 yaliyowafanya wafuasi wote kutawanyika na kusababisha taharuki miongoni mwao na muda mchache umeme ulikatika mji mzima na kuongeza hofu.
Tofauti na Mikoa mingine kama Tabora,Igunga na Sikonge ambapo alifanya mkutano kwa amani kisha wananchi wake kuruhusiwa kumsindikiza,polisi wa Mpanda walijipanga kila kona kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa.
MWANANCHI
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Shunga,Mkoani Kigoma wamedai kusomba matofali na kulima bustani za watu binafsi na walimu kuchukua fedha hizo.
Wakizungumza shuleni hapo juzi wanafunzi hao walisema taaluma yao inashuka kutokana na kufanyishwa kazi za kubeba matofali ya watu,kulima bustani za kabeji na mashamba ya miwa huku fedha zikiingia mifukoni mwa walimu wao.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Joseph John alikiri kuwepo kwa suala hilo na kwamba uongozi wa shule uliamua hivyo ili kupatikana fedha za kumlipa mlinzi anayelinda madawati mapya kutokana na wazazi kukataa kuchanga.
Alisema walimu wamekua wakifanya kazi kwenye mazingira magumu na hata chaki za kuandikia ubaoni hakuna na hadi sasa hawajui hatma ya shule hiyo baada ya uongozi wa juu kutowajibu lolote.
MWANANCHI
Jaji mkuu wa Tanzania Othman Chande amesema wamepeleka majaji14 Mkoani Tabora ili kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.
Uamuzi huo unatokana na Mkoa huo kuwa na kesi nyingi ambazo hazijasikilizwa mpaka sasa kama ilivyo kwa Mkoa wa Dar es salaam.
Akizungumza katika kikao cha majaji na watendaji wakuu wa mahakama jijini Mwanza jana Chande alisema lengo la kikao hicho ni kutathmni,kuona walipokosea na kujadili changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua.
“Tumepeleka majaji 14 Mkoani Tabora kufuatia mrundikano wa kesi katika Mkoa huo,hizo ni jitihada za kuikabili changamoto hiyo,tutazidi kufanya hivyo ili kuhakikisha tunapunguza tatizo hilo kama sio kumaliza kabisa”alisema Chande.
UHURU
Deni la zaidi ya bilioni90 ambazo Serikali inadaiwa na Bohari kuu ya Dawa ‘MSD’ limezidi kuibua balaa baada ya Wabuge kucharuka na kutaka Serikali kutoa kauli kuhusiana na deni hilo huku wakishauri bunge kuahirishwa.
Wakati hayo yakiendelea bungeni,utoaji wa huduma katika hospitali ya Taifa Muhimbili ‘MNH’ na hospitali nyingine umeanza kuimarika kwa huduma kuendelea licha ya kasoro ndogondogo ambazo zimekua zikiwakuta wagonjwa.
Naibu wa Wizara ya Afya na ustawi wa jamii Dk.Steven Kebwe alisema Serikali itaanza kuwasaka watumishi wa sekta ya afya wenye tabia ya kuuza dawa za Serikali kwenye maduka binafsi.
Alisema ukaguzi huo utakwenda sambamba na kuwabaini watumishi hao wa afya wanaomiliki vituo vya afya lakini dawa na vifaa wanavipata katika maeneo yao ya kazi.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Iringa linashikilia gari la kampuni ya Magazeti ya Mwananchi baada ya kulikuta na magunia mawili ya mirungi.
Kamanda wa Polisi Ramadhan Mungi alisem gari hiyo aina ya Nissan lilikamatwa November 10 lilipokua likitokea Dar kwenda Mbeya.
“Siku ya tukio askari walikua doria walilitia shaka gari hilo la Magazeti na walipolipekua walikuta magunia mawili ya mirungi yakiwa na mabunda302 .
Alisema gari hilo lilitoka Makao makuu ya kampuni ya Mwananchi saa 9 usiku na lilipofika Chalinze ndipo magunia hayo yalipakiwa na yalikua yakisafirishwa kwenda nchi za jirani.
HABARILEO
Kampuni ya Viettel ya Vietnam inayokua kwa kasi duniani ambayo inahamishia nguvu zake katika soko la Tanzania imetangaza ajira kwa wasomi wa Tanzania zaidi ya 2,000.
Viettel ambao uongozi wake wa juu ulikutana na Rais Kikwete akiwa ziarani nchini humo hivi karibuni na kuahidi neema kubwa kwa Watanzania katika sekta ya mawasialiano imetangaza nafasi hilo kupitia gazeti hili.
Wafanyakazi wanaohitajika ni wale wenye ujuzi katika masuala ya rasilimali watu ,sheria,fedha ,uhasibu,takwimu,uwekezaji,,ugavi,usafirishaji,utunzaji wa vifaa,umeme,simu,teknolojia,habari na mawasiliano,biashara,utawala na uhusiano wa umma.
Akiwa nchini Vietnam Kikwete alisema ndani ya miaka mitatu tangu kampuni hiyo kuanza shughuli zake hapa nchini kiasi cha vijiji 4000 ambavyo kwa sasa havina mawasiliano vitapatiwa huduma hiyo katika awamu ya kwanza.
NIPASHE
Huku akiwa ametangaza kulivua taji la Miss Tanzania Sitti Mtemvu anadaiwa kuandaliwa hati ya mashtaka kuhusiana na tuhuma za kudanganya umri ili kutimiza sifa za kushiriki shindano hilo ambalo fainali zake kitaifa zilifanyika Oktoba11 mwaka huu kwenye ukumbi wa Milimani City.
Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini RITA tayari wameshbabainisha kwamba Sitti alipata cheti kipya kmwa njia ya udanganyifu na sasa wanaendelea kuchunguza ili kubaini wale waliohusika katika kukipata cheti hicho ili wote waweze kushtakikwa pamoja.
Taasisi hiyo imechukizwa na sakata hilo na imepanga kuchukua hatua zinazostahili ili iwe fundisho kwa wote ambao wanania ya kufanya kosa la aina hiyo.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook