Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA), imesema uchumi wa Afrika kwa mwaka huu unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.9, ikilinganishwa na asilimia 3.6 za mwaka jana.
Akiwasilisha ripoti kuhusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika kwenye kikao cha 55 cha kamati hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora wa UNECA Bw. Adam Elhiraika, amesema ukuaji wa pato la jumla la bara la Afrika ulipungua kutoka asilimia 4.6 za mwaka 2021 hadi asilimia 3.6 mwaka 2022, lakini ukuaji huo unatarajiwa kurudi hadi asilimia 3.9 kwa mwaka huu.
Kudorora kwa uchumi wa dunia, kupanda kwa bei kunakochochewa na mgogoro wa Ukraine, mabadiliko ya tabia nchi na kuzorota kwa hali ya kimataifa ya kiuchumi na kifedha kumeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa mwaka jana.
Asilimia 3.9 inayotarajiwa ukuaji wa uchumi wa Afrika katika mwaka huu wa fedha unachangiwa zaidi na ukuaji katika kanda ndogo za Afrika mashariki, kaskazini na magharibi mwa bara hilo, alisema mkurugenzi huyo.
Elhiraika alisema mfumuko wa bei unatarajiwa kupungua mwaka huu huku mataifa ya bara hili yakitarajiwa kukaza sera zao za fedha ili kuhimili shinikizo la mfumuko wa bei.
Kupanda kwa gharama za kukopa na mzigo wa kulipa madeni kunaleta changamoto kubwa mbeleni, alisema Elhiraika, akionyesha kuwa uwiano wa deni kwa Pato la Taifa unakadiriwa kufikia asilimia 61.9 mwaka 2023.
Mfumuko wa bei katika bara zima unakadiriwa kupungua hadi asilimia 12 mwaka 2023 kutoka asilimia 12.8 mwaka 2022, alibainisha.