Watumishi wawili wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu wakikabiliwa na mashtaka mawili ikiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kujipatia zaidi ya Sh.milioni 13.9.
Washtakiwa hao ni aliyekuwa Katibu wa chama hicho Deus Seif na Mwekahazina Abubakar Allawi ambao walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Rashid Chaungu.
Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Imani Nitume alidai walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 3 hadi Novemba 6 mwaka 2018, Dar es Salaam.
Ilidaiwa kwamba, washtakiwa hao wakiwa watumishi wa CWT, walitumia madaraka yao vibaya na kujipatia Sh. 13,930,963 kwa manufaa yao wenyewe.
Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa, katika tarehe na eneo hilo washtakiwa hao walichepusha kiasi hicho cha fedha mali ya CWT, kwa kutumia nafasi walizo nazo.
Washtakiwa hao walipelekwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana likiwemo kila mshtakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslim Sh.Mil 3.487,400.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 17 kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hoja za awali.
https://youtu.be/YOrACc921gs