Pamoja na sheria kumlinda mtumiaji, pia zinatoa adhabu kwa makosa yanayotokana na matumizi mabaya ya huduma na bidhaa za mawasiliano. Matumizi mabaya ni pamoja na wizi na utapeli, vitisho na unyanyasaji na kutumia huduma kinyume cha sheria.
Baadhi ya makosa na adhabu zake kama zilivyo kwenye Sheria ni pamoja na kifungo jela, faini au vyote kwa matumizi ya laini ya simu bila kuisajili, kutoa taarifa za uongo wakati wa kusajili laini, kuruhusu laini itumike bila kusajiliwa, kutokutoa taarifa za kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu na kutumia simu na laini ya simu ambavyo vimeibiwa.
Sheria pia imeweka adhabu kwa wanaochakachua simu ili kuzibadili uhalisi wake; wanaofungulia simu zilizofungwa chini ya utaratibu wa Rajisi Kuu ya Namba Tambulishi na wanaotuma ujumbe wa vitisho, kunyanyasa, kunyanyapaa na kuudhi.
Ili kuendelea kumlinda mtumiaji wa huduma za mawasiliano, Serikali kupitia TCRA inatekeleza mambo mtambuka ambayo ni pamoja na kitengo cha kitaifa cha kushughulikia masuala ya usalama wa mitandao,mfumo wa anwani mpya za kitaifa na postikodi, mfumo wa rajisi kuu ya namba tambulishi na huduma ya kuhamia mtandao mwingine wa simu bila kubadili namba ya
simu ya kiganjani.