Top Stories

Tamko la BAVICHA baada ya Kamanda Mambosasa kukutana na Waandishi

on

Baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Lazaro Mambosasa kukutana na wanahabari leo September 15, 2017 na kugusia ishu ya Maombi ya Kitaifa ya Vijana yaliyoratibiwa na BAVICHA, Baraza hilo la Vijana wa CHADEMA limetoa tamko.

Kupitia kwa Katibu Mkuu wake Taifa, Julius Mwita, BAVICHA imetoa tamko baada ya Kamanda Mambosasa kutoa kauli zinazoonesha kuzuia maombi yao ya kufanya maombi maalumu akidai yatakuwa maandamano kinyume cha taratibu.

Taarifa hiyo inasomeka:

BAVICHA tumefuatilia kupitia vyombo vya habari kuhusu alichozungumza Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Lazaro Mambosasa kwenye mkutano wake na Waandishi wa Habari mchana wa leo ambapo amegusia kuhusu shughuli yetu ya Maombi ya Kitaifa ya Vijana (National Youth Prayers for Lissu) ambayo tumezungumza na vyombo vya habari leo na kusema kuwa yamepangwa kufanyika siku ya Jumapili tarehe 17.09.2017 kuanzia saa nane mchana.

Tumeshangazwa na kusikitishwa na kauli kadhaa alizozitoa akionesha kuwa amezuia maombi hayo kwa sababu alizodai kuwa yatakuwa ni maandamano na kinyume cha taratibu.

Tungependa kusema yafuatayo kutokana na kauli hizo;

Mosi, shughuli yetu ya Jumapili haijapangwa kuhusisha wala haitahusisha maandamano yoyote kama ambavyo SACP Mambosasa ametafsiri. Tumesema wazi katika taarifa yetu kwa jeshi hilo wilayani Kinondoni, kuwa shughuli ambayo tumeiandaa inahusu MAOMBI ambayo yatahusisha watu wa imani za dini mbalimbali ambao kimsingi hawawezi kukutana ndani ya nyumba moja ya ibada lakini wote hao wanaweza kukutana sehemu moja, mahali pa wazi na kuomba DUA/SALA kwa utulivu pamoja.

Pili, tunaelewa sheria na taratibu za nchi zinazosimamia mikusanyiko mbalimbali haziwapatii Polisi mamlaka yoyote ya kuzuia mikusanyiko au kutoa kibali cha mikusanyiko, bali sheria na taratibu hizo zimeelekeza wahusika wa shughuli hiyo kutoa taarifa Polisi na kueleza siku, mahali, muda na wahusika wa mkusanyiko husika.

Baada ya kusikia kauli ya SACP Mambosasa, tunatoa wito kama ifuatavyo;

i. Tunamsihi SACP Mambosasa apate nakala ya barua yetu ya taarifa kuhusu shughuli hiyo ambayo tumepeleka mamlaka za kipolisi kama sheria inavyoelekeza, ili aweze kutafakari uzito wa shughuli hiyo ya Maombi ya Kitaifa ya Vijana kisha alinganishe na kauli zake alizotoa leo.

ii. Wakati tukiendelea na maandalizi ya shughuli hiyo ikiwa ni pamoja na taratibu zote za mwisho kufanikisha shughuli hiyo ya KIIMANI na si ya kisiasa kama ambavyo SACP Mambosasa anataka kuonesha, tumeitisha kikao maalum cha dharura cha vijana wote wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Viongozi Kitaifa wa Vijana kwa ajili ya hatua za mwisho kufanikisha shughuli hiyo ya kumuombea Lissu ambaye hali yake bado ni mbaya akiendelea kuwa chumba cha uangalizi maalum Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya.

Wakati madaktari wanafanya kazi ya kutibu, tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu anayeabudiwa na watu wa madhehebu ya dini mbalimbali, anafanya kazi ya UPONYAJI kupitia MAOMBI.

Tunaendelea kuwakaribisha vijana, wanawake, wazee na wananchi wote wenye mapenzi mema na taifa letu na ambao wameguswa na tukio la kinyama na kikatili alilofanyiwa Lissu, katika viwanja vya TP Sinza, Dar es Salaam, kumuombea Mhe. Lissu na taifa kwa ujumla ili liepuke kuandamwa na dhambi ya matendo ya namna hiyo yanayodaiwa kufanywa na watu wasiojulikana ili tukiamini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kujibu kilio cha Watanzania kuwaanika watu hao waovu na kuyafanya majukumu ya polisi ambayo ni kazi ya mikono ya binadamu, kuwa rahisi.

_______
Julius Mwita
Katibu Mkuu
BAVICHA Taifa

BREAKING: Polisi waongelea mikusanyiko ya kumuombea Tundu Lissu

Soma na hizi

Tupia Comments