Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imetekeleza amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili, mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Sethi ili akafanyiwe vipimo.
Katika kesi hiyo, mbali na Sethi mshtakiwa mwingine ni James Burchard Rugemarila ambao wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi ikiwemo kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya USD 22, 198,544.60 na Tsh 309,461,300,158.27.
Hayo yamebainishwa na Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipotishwa kwa ajili ya kutajwa ambapo amedai kuwa wametekeleza amri waliyopewa na Mahakama ya kumpeleka Sethi Muhimbili na amefanyiwa vipimo, kinachosubiriwa ni ripoti ya Daktari.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Respicius Didus amedai kuwa kuna suala la ucheleweshaji upelelezi kwani washtakiwa walifikishwa Mahakamani June 19, 2017.
>>>”Washtakiwa wapo ndani na kila tukija katika kesi Jamhuri wanatuambia upelelezi haujakamilika. Wateja wetu wakiendelea kukaa ndani kuna athari sana.”
Hata hivyo, Wakili Swai akijibu hoja hizo alidai kuwa kesi hiyo ni ya kughushi na uchunguzi wake unachukua muda, hivyo Mawakili wajue upelelezi bado unaendelea.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi October 27, 2017.
Kilichojiri kesi ya Harbinder Seth na Rugemarila Mahakamani DSM!!!