Ijumaa, October 13, 2017 Mawakili wa utetezi wa aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Jamal Malinzi na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha, wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba hawaruhusiwi kuwaona wateja wao.
Aidha, imeelezwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo kwa upande wa TAKUKURU umekamilika na jalada hilo bado limekwama kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hayo yameelezwa na Wakili wa utetezi Richard Rweyongeza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Leonard Swai kueleza kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Rweyongeza amedai kuwa wiki iliyopita walipewa taarifa kuhusu uwepo wa jalada la kesi hiyo na wao hawana ugomvi na upelelezi, lakini wanapata taabu ya kuelewa kinachoendelea kwa DPP.
>>>”Tunaomba ahirisho fupi ili tuone kitatokea nini lakini hawasemi wamefuatilia na wamefikia wapi. Tunaomba hamasa iwepo ukizingatia makosa yao hayana dhamana, hivyo tunaomba ahirisho la wiki moja.”
Amedai kuwa hatua ya kuomba ahirisho fupi inatokana na wakati mgumu wanaoupata, ikiwemo kuzuiwa kuwaona wateja wao.>>>”Mawakili haturuhusiwi hata kuwaona na ni shida sana, hivyo ikishindikana tutarudi tena kwa DPP ili kuuliza.”
Naye Wakili Swai amedai kuwa pande zote mbili zilifuatilia kwa DPP ili kuhakikisha kesi hiyo inasikilizwa, hivyo wanaomba muda.
>>>”Tupeane muda wa wiki mbili ili tufuatilie kwani tukipata muda zaidi itakuwa rahisi kujua hatua iliyofikia.”
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi October 27, 2017 huku akiutaka upande wa mashtaka ufike na jibu sahihi ili ipangwe tarehe kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali (PH).
Washitakiwa wengine ni aliyekuwa Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na aiyekuwa Mhasibu wa Shirikisho hilo, Nsiande Mwanga ambao wanakabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418.
Meli ya kifahari kutoka OMAN ilivyoingia ZANZIBAR