Serikali ya Tanzania imesema kuwa ipo tayari kugharamia matababu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye yupo kwenye matibabu Nairobi baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana mchana wa September 7, 2017 akiwa nyumbani kwake Area D, Dodoma.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hayo alipokutana na Waandishi wa habari kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambapo alisema Serikali inasubiri kupata maombi kutoka kwa familia ya Lissu ikiambatana na taarifa rasmi kutoka kwa madaktari kuhusu mahitaji ya matibabu zaidi ya mgonjwa na itagharamia matibabu zaidi popote Duniani.
Waziri Mwalimu amesema Lissu ni Mbunge na Mtanzania hivyo Serikali inao wajibu wa kugharamia matibabu yake hadi apone ili aweze kuendelea na kazi ya kuwahudumia Watanzania na wana Singida Mashariki.
Aidha, Serikali imesisitiza kuwa iko tayari kuendelea kushughulikia matibabu endapo maombi ya kufanya hivyo yatawasilishwa rasmi Serikalini, ikiwemo kupata taarifa ya maendeleo ya afya yake kutoka kwa Madaktari wanaomhudumia Nairobi na itatakiwa kupatikana kupitia ridhaa itakayotolewa na mwenyewe Lissu au Mwanafamilia wa karibu kama taratibu za Kidaktari zinavyoelekeza.
Wakati huo huo, Waziri Ummy amesema Serikali imeshangazwa na dhana ya kuchangishana kwa ajili ya matibabu ya Lissu, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kutokea matapeli watakaochangisha Watanzania fedha kwa madai kwamba Mbunge huyo amekosa hela za matibabu.
Kama ulipitwa na Mbowe alivyoeleza Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi