Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema hadi kufikia Jumamosi ijayo, zoezi la kuzima laini zote za simu ambazo bado hazijasajiliwa kwa alama za vidole litakuwa limekamilika.
Aidha, TCRA imesema kuanzia Juni 30, 2020, mmiliki wa laini atatakiwa kuwa na laini moja tu ya simu kwa kila mtandao. Wenye laini zaidi ya moja (kwenye mtandao husika) watatakiwa kuchagua moja na zinazobaki zitazimwa.
Kanuni ya 18 na 19 ya Sheria za Kielektroniki na Mawasiliano ya Posta (Usajili wa Laini) ya mwaka 2020, inamtaka kila mtu kumiliki laini moja kwa mtandao mmoja wa simu kuanzia Juni 30, mwaka huu.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa TCRA, Frederick Ntobi, amesema zoezi la kuzima laini ambazo hapo awali zilikuwa zimesajiliwa kwa kutumia Kitambulisho cha Mpiga Kura na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi litafanyika kwa awamu mbili.
Ameongeza kuwa, laini takriban 8,722,527 zilizobakia kusajiliwa hadi tarehe 02/03/2020 zitakuwa zimezimwa rasmi kufikia Machi 14 mwaka huu.