Katika kusheherekea Siku ya Viwango Afrika kwa mwaka 2022, Shirika la Viwango tanzania (TBS) limeandaa shughuli mbalimbali ikiwemo Uandishi wa Insha kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kutoa elimu kwa maafisa wa Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhusu masuala ya Viwango.
Ameyasema hayo leo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mhandisi Johannes Maganga katika hafla ya Uzinduzi wa Mashindano ya Uandishi wa Insha kwa wanafunzi wa elimu ya Juu katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika Machi 2022.
Amesema kila mwaka Shirika la Viwango barani Afrika (ARSO) huidhinisha maudhui ya insha na hualika Mashirika ya Viwango barani Afrika kuandaa shindano la insha kwa vyuo vikuu katika ngazi ya kitaifa. Washindi watakao patikana watashindanishwa katika ngazi ya Afrika.
“Shirika la Viwango huratibu zoezi hili katika ngazi ya Taifa ambayo inahusisha kutoa matangazo kwa wanafunzi kushiriki, kupokea insha kutoka kwa washiriki na kutoa washindi wa insha”. Mhandisi Maganga.
Aidha amesema mashindano hayo ya uandishi wa insha ya ARSO yanalenga kuwawezesha vijana wa kiafrika kuelewa umuhimu wa viwango katika kuwezesha maendeleo endelevu barani Afrika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uandaaji Viwango TBS, Hamisi Mwanasala amesema kauli mbiu ya mwaka huu inatuelekezeka katika kutafakjari mchango wa viwango katika kuendeleza uchumi wa viwanda hasa kwenyye sekta ya madawa na vifaa tiba dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa UVIKO 19 ambao umekuwa tishio kwa nchi za Afrika na Dunia kwa ujumla pamoja na magonjwa mengine ya mlipuko yanayoweza kutokea wakati ujao.
Nae Kaimu Meneja Viwango Nasra Hussein amesema wanafunzi ni wadau wakubwa wa Viwango hivyo ni fursa pekee kuwatumia kama mabalozi kupitia insha watakazoandika kwa ajjili ya kuelezea manufaa ya viwango katika ngazi za kiuchumi, kijamii na kimazingira.