Upelelezi wa kesi ya kuchapisha video ya ngono kupitia ukurasa wa Instagram inayomkabili Msanii wa Filamu, Wema Sepetu umekamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Upelelezi huo umekamilika ikiwa ni miezi minne imepita tangu Wema alipofikishwa mahakamani hapo Novomber 1, 2018.
Hayo yameelezwa na Wakili wa Serikali, Glory Mwendi mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde.
Wakili Glory ameeleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kasonde ameahirisha kesi hiyo hadi February 21, 2019 kwa ajili ya Ph.
Katika kesi hiyo namba 322 ya mwaka 2018, Wema anadaiwa Oktoba 15 katika maeneo tofauti ya jiji la DSM alichapisha video za ngono kupitia ukurasa wake wa Instagram wakati akijua ni kinyume na sheria.
Wema yupo nje kwa dhamana, ambapo moja ya masharti aliyopewa ni kutochapisha/kutoweka picha ama maneno ya kingono katika ukurasa wake wa Instagram pamoja na kusaini Bondi ya Sh.Milioni 10.