Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu miaka 17 jela wafanyabiashara watatu akiwemo Raia wa China, Yang Feng Glan ‘Malkia wa Tembo’ baada ya kutiwa hatia kwa makosa ya kufanya biashara haramu ya Meno ya Tembo ikiwemo vipande 860 vyenye thamani ya Bilioni 13.
Washtakiwa wengine ambao ni raia wa Tanzania ni Salvius Matembo na Philemon Manase.
Hukumu hiyo iliyochukua takribani saa 5 ambapo ilianza kusomwa saa 9:57 asubuhi hadi saa 9 alasiri imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Hata hivyo, upande wa mashtaka kupitia Wakili wake Nehemia Nkoko amesema wateja wake wanatangaza nia ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Katika hukumu hiyo ambapo washtakiwa wapo mahabusu tangu mwaka 2014, Hakimu Shaidi amesema anatoa hukumu hiyo baada ya kuwatia hatiani washtakiwa katika kesi hiyo iliyokuwa na mashahidi 11.
Amesema licha ya washtakiwa kuwa wakosaji wa kwanza lakini wamesababisha hasara kubwa kwa uchumi wa taifa.
Amesema washtakiwa walijiingizia kipato kisicho halali na wamehujumu uchumi wa taifa na kulikosesha mapato, hospitali zimekosekanika, hakuna barabara nzuri hivyo jambo hilo halikubaliki.
Pia amesema mshtakiwa (Manase na Matembo) ni wasaliti wa nchi kwani waliamua kula wenyewe kwenye giza na sasa wameletwa kwenye mwanga.
Kuhusu mshtakiwa wa tatu (Yang Feng Glan), amesema yeye ni mgeni na amekaribishwa nchini lakini akafanya uhujumu.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Shaidi amesema mshtakiwa (Manase) mahakama inaamuru aende jela miaka 15.
Pia mshtakiwa (Glan) na wa pili (Matembo) nao wanahukumiwa kwenda jela miaka 15.
Pia kwa kosa la tatu, amesema mahakama inaamuru washtakiwa wote waende jela miaka miwili ama faini ya mara mbili ya Meno ya Tembo hayo ambayo ni sawa na Bil.27.
Pia mahakama hiyo imesema inaamuru mali zilizohusika katika shughuli za biashara hiyo haramu zitaifishwe ikiwemo nyumba ya Muheza Tanga na shamba.
Washtakiwa kwa pamoja, wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014 walijihusisha na biashara ya nyara za serikali.
Katika kipindi hicho washtakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 860 vya meno ya Tembo vyenye thamani ya Bilioni 13.9 bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.
Wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014 kwa makusudi raia wa China, Glan aliongoza na kufadhiri vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande hivyo 860 vya Meno yaTembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.
Kwa upande wa washtakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za serikali kwa kukusanya, Kusafirisha na Kuuza Meno ya Tembo kwa nia yakujipatia faida.
Ilidai kuwa Mei 21, 2014 katika eneo la Sinza Palestina wilaya ya Kinondoni mshtakiwa Manase alitoroka chini ya ulinzi halali wa askari wa Jeshi la Polisi D 7847 Koplo Beatus ambaye alikuwa akimshikilia kwa makosa yakujihusisha na biashara za nyara za serikali.
VILIO VYATAWALA MAHAKAMANI KISUTU, HUKUMU MALKIA WA TEMBO